Majaliwa ataka wadau wahusishwe mafuta

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametaka kuhusishwa kwa wadau mbalimbali wa masuala ya mafuta, zikiwemo taasisi za uagizaji mafuta nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alihoji mkakati wa serikali kutokana na sintofahamu ya upatikanaji wa mafuta katika vituo mbalimbali vya kuuza nishati hiyo hivi karibuni, ambapo mafuta ya petrol na disel yamekuwa hayapatikani katika baadhi ya maeneo, lakini bei ikishatangazwa yananza kupatikana, lakini pia alizungumzia suala la bei ya mafuta kubadiika mara kwa mara

Katika majibu yake Waziri Mkuu pamoja na kumuagiza Naibu Waziri Mkuu Dk Dotto Biteko kushughulikia jambo hilo, alitaka pia wahusishwe wadau mbalimbali wa masuala ya mafuta.

“Tuhakikishe kwanza nishati inapatikana katika vituo vyote na wakati wote, ili Watanzania waweze kunufaika na upatikanaji huu.

“Ni muhimu kuhusisha pia taasisi zote za mafuta ikiwemo EWURA, wanunuzi wa mafuta kwa mfumo wa bulk, taasisi ya ununuzi wa mafuta, tutengeneze kikao kikubwa na wizara kadhaa zinazohusika mfano Fedha, Ofisi ya Uratibu ya Waziri Mkuu, mkae pamoja muone namna ya upatikanaji wa mafuta.

“Suala la bei tutangalia hapo baadae kwa sababu huwa zinabadilika kutegemeana na upatikanaji, lakini tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta, ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa taifa letu.

“Na kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumepata majibu na tutawapa taarifa Watanzania,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button