Majaliwa atoa maagizo kuimarisha ushirika
DODOMA; SERIKALI imeiagiza Wizara ya Kilimo iimarishe na kufanya ufuatiliaji wa watendaji wa vyama vya ushirika ili wazingatie maadili ya utumishi wa ushirika, uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Pia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo na Tume ya Maendeleo ya Ushirika waharakishe na kusimamia utekelezaji wa mikakati iliyopitishwa hususani katika maeneo ya teknolojia ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo na masoko ya mazao.
Majaliwa alisema hayo alipozindua mdahalo wa upatikanaji mitaji ya fedha za maendeleo ya ushirika Dodoma jana.
Pia, aliwahimiza wakulima na wananchi kwa ujumla hakikisheni mnajiunga na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa, ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.
Majaliwa ameagiza taasisi za kifedha zikiwemo benki na mifuko ya maendeleo, waendelee kushirikiana na vyama vya ushirika kwa kuweka mifumo rafiki ya upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe maandiko ya taarifa zilizozinduliwa zinaandaliwa pia kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika nazo.
“Pia, wadau wote wa maendeleo, endeleeni kushirikiana na serikali katika kutoa rasilimali, utaalamu na ubunifu unaohitajika katika kuendeleza sekta hii muhimu,” alisema.
Majaliwa alisema sekta ya ushirika nchini inaendelea kuimarika ikiwa ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa katika maeneo mbalimbali.
“Hadi sasa, Tanzania inajivunia kuwa na zaidi ya vyama 7,000 vya Ushirika vilivyosajiliwa, vyenye jumla ya wanachama zaidi ya milioni nane. Vyama hivi vinajumuisha sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, uvuvi, madini, biashara na huduma za kifedha,” alisema.
Aliongeza: “Mafanikio haya tunayoyaona leo si ya Serikali pekee, bali ni ya ushirikiano wa wadau wote walioamini kwenye dira ya maendeleo ya taifa letu. Hivyo, ninawashukuru na kuwapongeza sana. Mafanikio ya sekta ya ushirika na kilimo yanahitaji mshikamano wa kitaifa, ushirikiano wa kweli na dhamira ya dhati kutoka kwa kila mmoja wetu.”



