Majaliwa atoa maagizo kulinda uchumi, uwekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni nguzo ya uwekezaji, mazingira ya biashara, ukuaji sekta ya madini, ujenzi wa miundombinu.
Ameiagiza isimamie mashauri kwa wakati, ufanisi, kwa muda mfupi na kwa kuzingatia misingi ya uzalendo na uadilifu.
Majaliwa alisema hayo Dodoma jana wakati wa maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mwaka 2018 na uzinduzi wa mafunzo kwa mawakili wa serikali.
Alisema ofisi hiyo ina jukumu kubwa hasa ikizingatiwa kuwa nchi ina wizara 22, halmashauri 184 na mashirika ya umma na taasisi za serikali zisizopungua 347.
“Ni ukweli usiopingika kuwa ofisi hii ni ya kimkakati na ina dhamana kubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ameanza kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake,” alisema Majaliwa.
Aliiagiza ifanye tathmini ya utendaji wao ili kubaini mafanikio na changamoto zinazowakabili hasa wanapoiwakilisha serikali katika mashauri.
Majaliwa aliipongeza kwa kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa kuwa na ofisi kwenye mikoa 17 ya Tanzania Bara na kwenye masijala za Mahakama Kuu zinazosimamia mashauri ya madai na usuluhishi kwenye mahakama za ndani na nje ya nchi.
Aliipongeza ofisi hiyo kwa kuokoa fedha ambazo serikali ingelipa kwenye asilimia 80 ya kesi ilizoshinda hadi jana.
“Ushindi huu ni ishara chanya kwa serikali katika kuhakikisha kwamba haipati hasara au kupoteza fedha nyingi kutokana na madai yaliyofunguliwa dhidi yake yanayosababishwa na watendaji au wataalamu wa serikalini kushindwa kuzingatia sheria na hivyo kusababisha kufunguliwa kwa mashitaka,” alisema Majaliwa.
Aliipongeza ofisi hiyo kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki kusimamia mashauri na akaagiza isomane na mifumo ya mahakama na wadau wengine ikiwamo ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Majaliwa ameiagiza ofisi hiyo kwa kushirikiana na wizara na idara za serikali watumie kila fursa ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya majadiliano na maridhiano ili kumaliza kesi ili kulinda mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara.
Aliagiza watendaji wa serikali wazingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa zikiwamo za usimamizi wa mikataba na makubaliano ili kuepuka migogoro inayosababisha serikali ishitakiwe.
Majaliwa ameagiza watendaji wa serikali waongeze umakini wanaposhughulikia masuala ya uwekezaji ili kujenga mazingira bora ya kuvutia uwekezaji.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ndani ya miaka mitano imeokoa fedha ya serikali Sh trilioni 7.6 ambazo ingetakiwa kulipa kama ingeshindwa kesi au mashauri mahakamani.
Dk Ndumbaro alisema ofisi hiyo imefanya kazi kubwa ya kushinda mashauri ya madai kwa njia ya majadiliano na usuluhisho kwa niaba ya serikali.



