Majaliwa atoa maagizo sekta ya nyuki ikuze uchumi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo manane ili kukuza sekta ya nyuki.
Majaliwa ametoa maagizo hayo Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani.
Alisema ni vema wizara ikashirikiana na wadau kutafuta fedha zitakazowezesha kutekeleza malengo ya mpango wa kuendeleza sekta hiyo ili kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji asali na kuifanya Tanzania ifanye vizuri katika sekta hiyo.
Majaliwa alisema pia, serikali imejipanga kujenga viwanda vinane vipya vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye mazao ya nyuki asali nchini.
“Uwepo wa viwanda hivi utatuhakikishia ubora wa asali zetu na viwango vya juu, kuongeza mauzo na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazohitajika kutoa huduma ya kusambaza asali duniani.”
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali kwa nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Katika bara la Afrika Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji asali, na duniani tumeshika nafasi ya 14. Takwimu zinaonesha Tanzania ni kati ya nchi chache zinazopata fursa na kunufaika kiuchumi na mdudu nyuki.”
Alisema sekta hiyo imekuwa na mchango kwa Taifa na imeajiri watu zaidi ya milioni mbili na imeingia kwenye masoko mbalimbali duniani ikiwamo Uingereza na China.
“Kumekuwa na ongezeko la mauzo ya asali ya Tanzania nje ya nchi, kwenye masoko mbalimbali na kumeongezeka hadi tani 431 kwa sasa, mazao ya nta tumeongeza ambayo tunauza nje ya nchi, soko hili ni kubwa lazima watanzania tuamue kuingia kwenye masoko na nta na asali.”
Majaliwa aliiagiza Tamisemi ihakikishe inashiriki katika utekelezaji wa mipango ambayo imezinduliwa na kuimarisha kitengo cha uzalishaji nyuki katika halmashauri zote katika wilaya ili huduma za wafugaji ziimarike.
Pia, aliutaka Mfuko wa Misitu Tanzania kuhakikisha unatenga fedha za kuviwezesha vikundi vya wafugaji asali na wajieleze walipo, namna ya kupata kilichopo katika mfuko na masharti yaangaliwe.
Majaliwa pia, aliuagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha mashamba makubwa ya kufugaji nyuki kibiashara kwa kuruhusu wanachi kufunga mizinga katika misitu ili kuongeza kiwango upatikanaji wa asali na uhifadhi nyuko.
Pia, aliitaka TFS kuwasaidia wananchi kwa kuwachongea mizinga bora ambayo haisababishi nyuki kuhama wanapoingia kwa kutumia teknolojia iliyowekwa, ikiwemo kuvuna vumbi la nyuki ambalo lina manufaa kiafya.
Majaliwa aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha maabara ya nyuki iliyopo Njiro Arusha inakuwa na vifaa vya kisasa vitakavyotosheleza mahitaji ya wataalamu.
Pia, alitaka wizara hiyo ikidhi mahitaji na ubora wa asali inayotakiwa ili wananchi waitumie vizuri na maabara hiyo kushirikiana na Wizara ya kilimo kuimarisha matumizi ya mazao yanayoweza kuleta nyuki ili kupata mbegu bora.
Pia, aliagiza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kufanya utafiti kimkakati ambazo zitatoa matokeo ili ziwe na manufaa shambani, walaji.
Majaliwa aliitaka TFS na Tafori kuanzisha vituo vya kusalisha makundi ya nyuki ngazi za halmashauri ili zitumie fursa ya uwepo wake na yalete manufaa.
Pia, aliitaka TFS kuanzisha ghala la kuhifadhia asali nchini lenye kipozeo (mtambo baridi) ili asali idumu kwa muda mrefu na iwe yenye kiwango.
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda aliwataka vijana watumie fursa ya uwepo wa nyuki kujishughulisha na ufugaji wake nyuki na kusaidia ni kwa nini mazao yake yanaimarisha nchi kiuchumi.
“Katika sekta ambazo nafikiri ni rahisi zaidi ni ufugaji wa nyuki, jaribuni kujifunza juu ya mdudu huyo na msaidie kueleza ni kwa nini tunampa nafasi kubwa namna hii. Mazao yake yanayotokana na nyuki kiuchumi nayo yanatuimarisha sana,” alisema Pinda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alisema sekta ya ufugaji nyuki bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kiwango kidogo cha uzalishaji wa asali ikilinganishwa na uwezo uliopo.
“Kiwango kidogo cha asali kinachouzwa katika masoko ya nje ya nchi, kuendelea kwa matumizi ya mzinga ya asili ambayo huchangia katika uharibifu wa misitu, uvamizi wa maeneo ya hifadhi ambayo ndiyo makazi ya asili ya
nyuki na matumizi ya viuatilifu vinavyoathiri afya ya nyuki,” alisema Dk Chana.
Aliongeza: “Kutokana na changamoto hizi, Wizara kwa kushirikiana na wadau tumekuja na mpango wa kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki ya Tanzania Iliyo bora.”



