Majaliwa awapongeza Yanga

DODOMA — Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepongeza mchango wa michezo nchini huku akizitaja klabu za Yanga na Simba, pamoja na timu za taifa, kuwa mabalozi wakubwa wa Tanzania barani Afrika na duniani.
Akihitimisha mkutano wa Bunge, Majaliwa aliipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa 31 wa Ligi Kuu na Simba kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF. Alisema mafanikio haya ni chachu ya maendeleo ya michezo nchini.
“Niipongeze sana Klabu ya Simba kwa hatua kubwa ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika,” alisema Majaliwa huku akiwatakia mafanikio zaidi.
Aliwapongeza pia wanamichezo wengine akiwemo Alphonce Simbu, na timu za wanawake za Futsal, CECAFA na Basketball kwa mafanikio yao ya kimataifa.
Majaliwa alieleza kuwa serikali imewekeza kikamilifu katika maandalizi ya CHAN 2025 na AFCON 2027, ambapo ukarabati na ujenzi wa viwanja unaendelea kwa kasi kubwa.