Majaliwa kubariki Mkutano Mkuu TOA

ARUSHA; Waziri Mkuu kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA), unaotarajia kufanyika mkoani Arusha kuanzia Juni 12 – 14, 2024.

Akizungumza mjini hapa, Mwenyekiti wa TOA na Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, amesema mkutano huo utafanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ukibeba dhima ya uboreshaji na utendaji kazi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Amesema mkutano huo utahusisha Makatibu Tawala wa mikoa yote 26, Wakurugenzi watendaji wa majiji, miji na halmashauri zote 184, huku wakiwalika na Maofisa Utumishi wa Sekritarieti za mikoa na halmashauri zote nchini pamoja na wakurugenzi wa Manispaa zote na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa upande wa Zanzibar, lengo likiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja na kubadilishana uzoefu katika utoaji huduma kwa wananchi kupitia Maamlaka hizo.

“Mkutano huu una lengo la maboresho ya Serikali za Mitaa katika masuala ya ugatuaji wa madaraka kwenda kwa wananchi, ukiwemo ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma za kijamii, ikiwemo maji, kilimo, afya, miundombinu, usimamizi wa rasilimali watu, fedha na utawala bora,” amesema Msovela

Amesema umoja huo ulianza mwaka 2002 kwa kushirikiana na Serikali ya Japani, kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) ambapo watumishi zaidi ya 6,000 wamenufaika kwa kupata mafunzo kupitia TOA.

 

Habari Zifananazo

Back to top button