WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mashindano ya kimataifa ya Kurani yanajenga jamii yenye maadili, pia yana manufaa kwa uchumi.
Majaliwa alisema hayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana kwenye kilele cha mashindano hayo yaliyohitimishwa kwa washiriki kusoma Kurani na kuonesha uwezo wao wa kuhifadhi kitabu hicho kitakatifu.
“Mashindano haya yanaipa fursa Tanzania kujitangaza kimataifa kwenye dini na utamaduni wake lakini pia kwa kuwa mwenyeji kunaifanya nchi iongeze uchumi wake kupitia sekta ya utalii, biashara na huduma,” alisema.
Majaliwa alisema mashindano hayo kufanywa nchini, yametoa nafasi ya nchi kujitangaza duniani pia kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mengine, kushirikiana na nchi zilizoshiriki kwenye masuala ya maendeleo.
Alisema kupitia mashindano hayo, wageni wengi kutoka mataifa tofauti duniani wameshiriki na Watanzania wametumia fursa hiyo kufanya biashara ya vitu mbalimbali uwanjani hapo lakini pia kwenye maeneo ya huduma.
Alisema mashindano hayo yanatoa mwanga, ukweli na mwongozo wa kila siku katika maisha ya jamii hususani ya Kiislam hivyo mashindano hayo ni sehemu muhimu kuhamasisha jamii hasa vijana kuendelea kujifunza na kuhifadhi Kurani.
Akitaja faida za mashindano hayo, Majaliwa alisema vijana kushiriki kunawapa fursa ya kuimarisha uhusiano wao na Mungu na kupitia ujuzi wa Kurani, yanahamasisha utamaduni wa kujisomea na kuhifadhi kitabu hicho kitakatifu.
“Hali hiyo inachangia utamaduni wa kuheshimu dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii,” alisema Majaliwa.
Faida nyingine ya mashindano hayo ni kuwawezesha vijana na watoto kuonesha uwezo wao katika usomaji na kuhifadhi kitabu hicho kitakatifu na kuwa fursa kwao kukuza vipaji, kujivunia mafanikio yao na kujenga nidhamu ya uwajibikaji.
Alisema mashindano hayo hutoa nafasi ya kujenga maadili bora kama vile uadilifu, uaminifu na kitendo cha kujitolea wakati wote.
Alisema pia mashindano hayo hutangazwa kwa mataifa mengi na kutoa fursa kwa Waislamu kuungana kwa malengo ya umoja.
Majaliwa alitaka mashindano hayo yatumike kuendeleza misingi ya dini, maadili na amani.
Wakati huo huo, waziri mkuu aliwatakia Waislamu mfungo mwema wa Ramadhani akihimiza wautumie kuombea taifa amani.
Akizungumzia matarajio ya serikali, Majaliwa alisema ni kuona elimu hiyo inatolewa kuanzia ngazi ya chini ili kuwaandaa watoto kushiriki kusoma Kurani.
“Nahamasisha jamii kuanzisha madrasa kwenye maeneo yetu ili wajifunze na hasa kwenye eneo la kuhifadhi kitabu hicho ili kuleta maendeleo ya kiroho, serikali itaendelea kushirikiana na jamii kuendeleza mashindano hayo,” alisema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, aliitaka jamii kuendeleza maadili akisisitiza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania.
“Wito wangu kwa viongozi wa madhehebu ya dini ni kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini katika shule, vyuo na taasisi mbalimbali za utoaji elimu hiyo. Hatua hii itaendelea kutoa fursa kwa watoto wetu na vijana kupata elimu ya dini na kuwaandaa kuwa watu wema,” alisema Majaliwa.
Pia, aliwataka Watanzania kuhamasisha amani na utulivu. Alitaka madhehebu ya dini yaendelee kuhimiza jambo hilo kwa waumini wao.
Pia, alisisitiza mshikamano na utulivu wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema wakati huu ambao Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea kuboresha daftari la wapiga kura, kila Mtanzania atumie fursa hiyo kuboresha taarifa zake ili kuwa na uhakika wa kushiriki uchaguzi huo.
“Niwaombe viongozi wa dini tutumie nyumba za ibada kuhamasisha waumini wetu wajiandikishe na washiriki kwenye mikutano na siku ya kupiga kura wajitokeze kuchagua viongozi wawatakao au wawanie nafasi za uongozi,” alisema Majaliwa.