Majaliwa mgeni rasmi miaka 100 Rotary District 9214

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kihistoria la Rotary District 9214 litakalofanyika Dar es Salaam kwa siku mbili.
Rotary District 9214 inaunganisha mataifa ya Uganda na Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Rotary District 9214 imesema mkutano huo utaendesha mijadala mbalimbali inayohusiana na huduma za taasisi hiyo kwa takribani karne moja sasa.
Aidha, taarifa hiyo imesema uwepo wa Waziri Mkuu leo na kesho kunaonesha namna taasisi hiyo ilivyokuwa karibu na wananchi katika kufanikisha maendeleo ya kitaifa na kuleta mabadiliko chanya kwa jamii za Tanzania na Uganda.
Chini ya kauli mbiu “Karne ya Huduma. Mustakabali wa Matumaini,” mkusanyiko huu wa kihistoria utawaunganisha wanachama wote wa Rotary, viongozi na washirika.
“Hili si kongamano la kawaida; ni sherehe ya kihistoria ya miaka mia, ushuhuda wenye nguvu wa karne ya kujitolea bila kuyumba, uongozi wenye mageuzi, na athari kubwa iliyosukwa katika kitambaa halisi cha jamii za Afrika Mashariki,” ilisema taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Gavana wa Rotary District 9214, Agnes Batengas alisema:”Kongamano hili linasherehekea urithi wetu wa pamoja na linafanya upya ahadi yetu ya kuleta mabadiliko yenye maana na ya kudumu kupitia huduma ya Rotary.”
Mwakilishi wa Rotary District 9214, Joseph Ssengooba alielezea haja ya kuungana pamoja kusherehekea uwapo wa taasisi kwa miaka 100 ikiongoza kwa ujasiri.
Katika kongamano la miaka 100, mhadhara mkuu utatolewa na mwakilishi wa Rais wa Rotary Kimataifa (RIPR), Bryn Styles unaoptarajiwa kutoa maarifa na mitazamo muhimu kutoka kwa mtandao wa kimataifa wa Rotary.
Kongamano pia litakuwa na mada iliyopewa jina la: “Kutoka Migogoro Hadi Kuishi Pamoja,” iliyoandikwa Dk Gladys Zikusoka. Mada hii itachunguza fikira kuhusu nafasi ya Rotary katika kukuza amani na uelewano.



