Majaliwa mgeni rasmi tuzo za Wanamichezo Bora 2024

DAR-ES-SALAAM : WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya tuzo za Wanamichezo Bora kwa mwaka 2024, zitakazofanyika Juni 1, 2025 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), zikiwa ni mara ya tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Mkumbukwa Mtambo, alisema tuzo hizo zimekuwa na mafanikio makubwa mwaka hadi mwaka, na zimeongeza ari kwa wanamichezo kushiriki mashindano ya kimataifa kwa bidii zaidi.
“Kwa mwaka huu kutakuwa na vipengele 20 vya tuzo, ambavyo viwili kati yake vimeboreshwa. Kimojawapo ni Sports Legend Award kwa ajili ya kuwatambua wanamichezo wastaafu waliotoa mchango mkubwa katika michezo,” alisema Mtambo.
Kipengele kingine kilichoboreshwa ni People’s Choice Award, ambacho kitawawezesha mashabiki kushiriki moja kwa moja kwa kupiga kura kumpigia mchezaji wanayempenda kwa kuandika jina lake na kulituma kupitia namba ya simu +255 689 525 363.
SOMA: Osimhen atwaa tuzo mchezaji bora Afrika
Mtambo alieleza kuwa lengo la kipengele hicho ni kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa utoaji wa tuzo pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya wanamichezo na mashabiki wao.
Hafla ya tuzo hizo inatarajiwa kuwa ya kipekee mwaka huu, ikitarajiwa kuvutia wadau mbalimbali wa michezo, huku ikiendelea kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya michezo nchini.