WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema Serikali imepanga kutumia Shilingi milioni 500 kuboresha tenki la maji lililopo kata ya Mkata liweze kuwahudumia wananchi wa kijiji cha Manga kilichopo, Wilayani Handeni Mkoa wa Tanga kwa kuhifadhi maji kutoka Bonde la Wami/Ruvu.
Waziri Aweso amesema hayo wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano Mkoani Tanga ambapo amesema kuwa tenki hilo lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita laki tano za maji linatakiwa liwe suluhu kwa wananchi wa Manga na maeneo yote ya Mkata.
SOMA: Aweso: Dawasa mkipiga chafya nchi nzima inaugua mafua
Amesema malengo ya serikali kutekeleza mradi wa maji Wami /Ruvu ni kuhakikisha huduma ya maji inafika na kutumiwa na wakazi wa eneo la Manga lililopo mpakani mwa wilaya za Handeni na Bagamoyo.
“Niwaelekeze DAWASA hakikisheni hawa wananchi wa Manga wanapata maji muda wote badala ya kwa mwezi mara mbili au tatu kwani hiyo sio dhamira ya Rais Samia ambayo anataka wananchi waweze kupata huduma karibu na maeneo yao “amesema Waziri Aweso.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dk. Batilda Burian amemshukuru Waziri Aweso kwa juhudi zake za kupambania sekta ya maji kwa kujitoa na ubunifu wake.
Ameongeza kuwa asilimia ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini imeendelea kuongezeka siku baada ya siku kutokana na juhudi za Serikali.