DAR ES SALAAM: SERIKALI imeziagiza Mamlaka za Maji nchini kuwaunganishia maji wananchi wenye uhitaji kwa mkopo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso leo Novemba 17,2023 katika hafla ya utiaji saini utekelezaji wa mradi wa maji eneo la Kusini mwa Mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama mradi wa Bangulo.
Amesema mkakati wa serikali ni kusambaza maji kwa asilimia 95 kwa mijini na asilimia 85 kwa vijijini ifikapo 2025.
“Mwananchi anayetaka kuunganishiwa maji muhakikishe ndani ya wiki mbili kashapata huduma, hata kama hana hela muunganishieni kwa mkopo mumkate kidogo kidogo anapolipa bili yake ya maji,” amesema.
Mradi huo wa Bangulo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ( Dawasa) unagharimu Sh bilioni 40 unatarajiwa kunufaisha wananchi 450,000.
Aweso amesema upatikanaji wa maji mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 kwa mjini umepanda kwa wastani asilimia 88 na inatarajia kufika asilimia 91 mwezi Desemba 2023, wakati kwa upande wa vijijini hali ya huduma imeongezeka kutoka asilimia 77 na inatarajiwa kufika asilimia 80 mwezi Desemba mwaka huu
“Dawasa mkipiga chafya nchi nzima inaugua mafua, hampoi, hamboi, nawapenda mpaka naumwa, mtoto akifanya vizuri kazi ya mzazi ni kumuombea dua tu, naamini mradi huu utatekelezwa na kumalizika kabla ya muda, ” amesema na kuongeza
“Mkandarasi alipwe fedha kwa wakati, vijana ambao wanaishi mradi unapotekelezwa wapewe ajira, mkiaminiwa aminika sio mnaiba sementi, mara misumari, “amesema
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Dawasa, Kihula Kingu alisema mradi huo utanufaisha wananchi wa Wilaya tatu za Ubungo, Temeke na Ilala na majimbo manne ya uchaguzi Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba na Ilala.
Amesema, awamu ya kwanza ya mradi itanufaisha wananchi wa Kata za Kwembe, Kitunda, Pugu Stesheni, Kipunguni na Mzinga.
Awamu ya pili ya mradi itanufaisha wananchi wa Kata ya Kivule, Kinyerezi, Zingiziwa, Majohe, Charambe, Kwembe, Buza, Msongola, Msigani na Mbezi.