Majibu yatakiwa kukosekana kwa umeme, maji

MEYA wa Manispaa ya Ubungo Mkoani Dar es Salaam, Jaffary Nyaigesha ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kueleza wananchi kinachosababisha kukosekana kwa huduma hizo katika maeneo waliyopo.

Nyaigesha ameagiza hayo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo.

Akitoa ufafanuzi katika hilo, Ofisa Huduma kwa Wateja Dawasa Kibamba, Julian Saimon amesema changamoto za maji katika wilaya ya Ubungo, zinatokana na hitilafu za umeme zinazojitokeza hivi sasa kwa sababu wao na tanesco wanategemeana.

Advertisement

Anasema umeme unapokatika unasababisha kukosekana kwa maji ama kupungua utoaji wake.

Kutokana na majibu hayo, Nyaigesha aliitaka Dawasa kubuni teknolojia ambazo hazihusiani na Tanesco ili umeme ukikatika usiathiri eneo hilo.

Naye Meneja Tanesco Wilaya ya Kimara, Jamal Kimolo amekiri kuwepo na changamoto za kukatika kwa umeme.

“Kituo cha Ubungo kinaangalia uzalishaji na matumizi ya umeme nchi nzima. Rais alitoa miezi sita kuhakikisha changamoto ya umeme imeisha, ambapo mwisho wa miezi sita ni mwezi huu wa pili.

” Tuna miradi 24 tuliyofanya ya kuhakikisha umeme haukatiki, inasaidia kuboresha umeme,” amesema na kuongeza baada ya siku chache tatizo la umeme litaisha.

Mwisho

/* */