Majiko ya gesi kutolewa bei ya ruzuku Longido

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza usambazaji wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku wilayani Longido mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia 2024-2034.

Mhandisi wa Miradi wa REA, Kelvin Tarimo amesema hayo wakati wa mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Longido na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa uliokua na lengo la kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali wilayani humo leo.

“Tupo hapa wilayani Longido kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kuanza rasmi uratibu wa mradi wa kusambaza na kuuza majiko ya gesi (LPG) ya kilo 6 ambapo kwa Wilaya ya Longido pekee jumla ya majiko 3,255 yatauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50,” amesema Mhandisi Tarimo.

Advertisement

Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Dk Kiruswa ameipongeza REA kwa kutekeleza miradi yake kwa ufanisi ambapo alisema kwa wilaya hiyo ya Longido hadi sasa vijiji vyote 51 vimefikishiwa umeme na kazi inaendelea ya kuunganisha vitongoji.

Katika hatua nyingine Tarimo amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inalojukumu la kuhakikisha Watanzania wanaachana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama kama ambavyo imeelekezwa katika mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akitoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni fursa.

“Wakala unatoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo ya kiuchumi na pia kupikia kwani umeme ni moja kati ya nishati rafiki kwa matumizi ya kupikia,”amesisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Longido wamepongeza jitihada za Serikali za kuwasambazia nishati safi ya kupikia ambapo wamesema kuwa  ni hatua nzuri ya kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.

Sinyati Yohana mkazi wa Kata ya Ketumbeine amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea kero wananchi wa Longido hususani wanawake na watoto kwa kutembea umbali mrefu kusaka kuni kwa ajili ya kupikia.