Mradi wa uchorongaji visima gesi asilia Mtwara unavyonufaisha wazawa

Hadi sasa zaidi ya Watanzania 320 wamepata ajira, wengine wakipata zabuni za Sh bil 20/-

MTWARA: Zaidi ya Watanzania 320 wameajiriwa katika nafasi mbalimbali  huku wengine wakinufaika kupitia zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 20 zinazotokana mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaoendelea katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo mkoani Mtwara umeleta

Hayo yameelezwa na Mhandisi Fabian Mwose kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) baada ya timu ya mamlaka hiyo kuzuru mradi huo kuona utekelezaji wake unavyoendelea.

Mhandisi Mwose amesema kuwa mradi huo unaohusisha uchorongaji wa visima viwili vya uzalishaji na kimoja cha utafutaji ulianza kutekelezwa Februari 06, 2026 ambapo hadi kufikia Juni 05, 2026, uchorongaji wa visima viwili vya uzalishaji vilivyopewa majina ya MB5 na MS2 ulikuwa umekamilika na uchorongaji wa kisima cha tatu kilichopewa jina la KASA-1X ulikuwa unaendelea.

“Miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kufuatia utekelezaji huo ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Mnazi Bay ambapo kisima cha MB5 kimeongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 40 kwa siku na kisima cha MS2 ambacho bado kinafanyiwa majaribio kinatarajiwa kuongeza ujazo mwingine zaidi wa uzalishaji wa gesi asilia,” Mhandisi Mwose aliongeza.

Kwa mujibu wa mhandisi huyo wa PURA, ongezeko hilo la uzalishaji wa gesi asilia umewezesha uwepo wa gesi zaidi kwa matumizi ya uzalishaji umeme, viwandani, majumbani na vyombo vya usafiri vikiwemo magari na pikipiki za miguu mitatu).

Kwa upande wa uwekezaji, Mwose alisema kuwa utekelezaji wa mradi huu pamoja na miradi mingine ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia inayoendelea umeongeza imani kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi kuhusu uhai wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini.

Kukamilika kwa mradi huu wa uchorongaji wa visima vitatu kutaifanya Tanzania kuwa na idadi ya visima 99 vilivyochorongwa tangu kuanza kwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kutoka visima 96 vilivyokuwepo awali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button