Makalla: CCM hatucheki na mtu katika kushika dola

KATIBU wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) , Itikadi, Uenezi, Siasa na Mafunzo, CPA Amos Makalla amesema Chama hicho hakicheki na mtu katika kushika dola na katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wamejipanga kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.

CPA Makalla ameyasema hayo leo Movemba 23,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka.

Makalla amesema kuwa kwa sasa Chama hicho kimeendelea kufanya kampeni za Uchaguzi huo na walizindua kampeni zao rasmi Novemba 20, mwaka huu katika mikoa yote nchini na yote ni kutaka kuhakikisha wagombea wa chama hicho wanashinda kwa kishindo.

Advertisement

“Katika uchaguzi huu wa Serikali ya Mitaa tutashinda na tunataka ushindi wa kishindo, kwa jinsi ambavyo CCM tumejipanga ni sawa na kusema yajayo yanafurahisha,”amesema CPA Makalla.

Aidha, Makalla amesema kwenye Wilaya ya Ubungo kuna mitaa 60 na katika jimbo hilo la Kibamba kuna mitaa 44 na kote wamehakikisha wameweka wagombea wazuri na wenye sifa.

“Kazi ya Chama cha siasa kilichosajiliwa ni kuhakikisha kinashika dola maana kazi ya kuhubiri kwenda mbinguni hiyo inafanywa na viongozi wa dini.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kushika dola ndio maana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa CCM imeweka wagombea wake kwa asilimia 100 katika kila nafasi kwani hakuna Mtaa,Kijiji Wala Kitongoji ambacho wameacha wazi.

“Vyama vingine havina utayari na ndio maana wameshindwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote na mpaka sasa kuna Mitaa ambayo tayari wagombea wake hawana washindani,” amesma CPA Makalla

Aidha, amewataka wananchi kutokubali kudanganyika na kuachana na propaganda na badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura.