Makalla: Wapinzani wanahamia CCM kwa kasi

Amos Makalla

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuna kasi kubwa ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kukimbilia chama hicho kutokana na utekelezaji mzuri wa ajenda zenye mvuto kwa vyama vya upinzani.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema hayo jana Dodoma alipohojiwa kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania chenye mada ya Kuelekea Mkutano Mkuu wa CCM, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1.

Makalla alisema kutokana na uongozi bora wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi, CCM imevuna wanachama wengi vijana hali inayofanya kuwa na wanachama wanaofikia zaidi ya milioni 10.

Advertisement

Alisema chama kimefanikiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 kwa asilimia kubwa kutokana na uharaka wa Rais Samia kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kutokana na ufanisi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, wananchi waliamua kukipa ridhaa chama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

“Ushindi wa kishindo wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, ni ishara nzuri kuwa wananchi wameridhishwa na sera, itikadi na utekelezaji wa ilani ya chama,” aliongeza Makala.

Kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kufikisha miaka 61, Makalla alisema Zanzibar imeandika historia yake yenyewe na ni kitendo cha kizalendo na cha kujivunia.

Alifafanua Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa lazima yafanyike ili kuondoa unyonge, manyanyaso, dhuluma na ubaguzi kutoka kwa wakoloni ili kuboresha huduma za kijamii kama maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Mkutano Mkuu wa CCM unatarajiwa kufanyika Januari 18 na 19, mwaka huu mkoani Dodoma na miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kufanyika ni kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara baada ya Abdulrahman Kinana kuomba kupumzika.

Kabla ya kushika nafasi hiyo, Kinana alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na serikali ikiwamo ya Katibu Mkuu wa CCM.