Makocha Simba, Coastal wategana

Kaimu Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro.

WAKATI muda wa kipute cha Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Coastal Union ukikaribia, makocha wa timu hizo wametegana kuhusu mbinu za vikosi vyao katika mchezo huo Oktoba 4.

Walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari leo kuelekea mchezo huo kwenye uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Kaimu Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema licha ya Simba kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa kuliko timu yake lakini wataingia uwanjani na mbinu za kuwashangaza wapinzani wao.

Advertisement

Kocha Joseph amesema Simba wana wachezaji zaidi ya watano wenye uwezo mkubwa na kuwapa matokeo kuwazidi Coastal Unioni, akidai wana mchezaji mmoja anayeweza kuleta matokeo tofauti kwa timu yao.

“Hatutakurupuka tunaingia kwa tahadhari, tumeimarisha safu ya ulinzi kwa kuwa washambuliaji wa Simba wanauchu wa kufunga,”amesema Lazaro.

SOMA: Simba presha inapanda, inashuka

Ameongeza kuwa katika mchezo huo kila mmoja anataka matokeo na kwamba Coastal inahitaji mkubwa zaidi na licha ya ubora wa Simba lakini ameona mapungufu yatakayowapa matokeo.

Lazaro amesema watacheza kwa tahadhari kubwa lakini pia watafanya mashambulizi kwa kushtukiza kwa ajili ya kutafuta pointi muhimu.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu David.

Naye Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu David amesema mchezo dhidi ya Coastal utakuwa mgumu.

Amesema amewatazama wapinzani wao katika mechi walizocheza siku za karibuni wamekuwa wakibadilika kiuchezaji na kushambulia kwa kasi kitu ambacho watachukuwa tahadhari.

“Ninatarajia kuwepo kwa mabadiliko kadhaa ya wachezaji kutokana na ratiba kuwa ngumu tumecheza mechi tatu ndani ya wiki moja, siwezi kusema nitampanga mchezaji gani au nani hatakuwepo kesho kwa kuwa tunatengeneza uwiano wa wachezaji.”

“Kuelekea Desemba ratiba itakuwa ngumu zaidi malengo yetu ni kushinda kila mchezo hauwezi kuwa bingwa kwa kushinda mechi nne, tunatakiwa kuendelea kukusanya pointi na tunaweza kuzuia vizuri,” amesema Kocha Fadlu.

Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein.

Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein amesema kwa upande wao wapo tayari kufuata maelekezo watayopewa kusaidia timu kupata ushindi.

“Wachezaji tupo tayari , tunaiheshimu Coastal kutokana na ubora wao lengo letu ni kuhakikisha tunashinda tukiwa nyumbani na kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Hussein.