Makonda asisitiza haki kwa wote

MWANZA: CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewataka watumishi na watendaji wa serikali kote nchini kuwa waaminifu katika kutoa huduma bora kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake pasipo kudhulumiwa.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, itikadi na uenezi, Paul Makonda alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mwanza.

“Haijalishi mtu upo ofisi gani jitahidini kuwathamini watu kwa utu wao na si kwa kuwadharau watu wengine na kuchagua wa kuwaheshimu kisa cheo au pesa binadamu wote ni sawa na wanastahili kuhudumiwa vizuri na si kuwadhulumu haki zao,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa “tuwatendee watu mazuri kila unayekutana naye hakikisha unamthamini si kwasababu anakupa pesa bali kwasababu ameumbwa kwa mfano wa Mungu ipo siku unayemtendea mabaya utamkuta amekaa mahali pazuri,” alisema.

Alisema CCM haipendi mtu anayemuheshimu mtu kwasababu ya cheo au pesa bali inataka kila mtu hapatiwe huduma bora kwa kupewa haki anayostahili.

“Unaweza kwenda kwenye ofisi fulani unajieleza kwasababu ni haki yako lakini hakuna anayekusikiliza wala kuhudumia lakini kiongozi akipiga simu nataka fulani mumsikilize utaambiwa samahani njoo njoo unapewa na kiti na chai, niwaombe Watumishi Nchi nzima haijalishi upo kwenye ofisi gani mthamini Mtu kwa utu wake,” alisema.

Makonda alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla kukaa na wakuu wote wa mikoa ya Kanda ya ziwa kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza utalii kanda ya ziwa.

Aidha Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa alipopigiwa simu na Kiongozi huyo kupata ufafanuzi wa kukamilika kwa ujenzi wa jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza alisema changamoto ilikuwa ni kupata mkandarasi wa kumalizia kujenga lakini kwa sasa wameshampata mkandarasi

“Hadi sasa tunavyoongea mkandarasi ameshapatika na tunatarajia kusaini mkataba baada ya wiki mbili na mkataba utasainiwa hapo hapo mjini Mwanza na Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa Sh bilioni 21 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la abiria na tunatarajia hadi kufikia Novemba 2024 Watanzania na wageni wote kutoka mataifa mbalimbali wataanza kulitumia jengo hilo,” alisema Makamba.

Mokonda aliwaomba wakazi wa Mwanza kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo kwasababu wanapokuza ushirikiano katika maendeleo wanarudisha upendo na ushirikiano kwa Mwenyekiti wa chama.”Umoja na ushirikiano wenu ndio msingi utakaowafanya muendelee kupata mema kutoka kwa mwenyekiti wa chama kwasababu mkishirikiana na kwa upendo mtafanya kazi kwa bidii na Rais Samia atawatekelezea mahitaji ya maendeleo yenu kwasababu atakuwa na huwakika kwa utekelezaji wa miradi,” alisema Makonda.

Habari Zifananazo

Back to top button