Makonda azindua shule Ukerewe

MWANZA; Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amezindua Shule ya Msingi Butiriti iliyopo wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makonda amesisitiza umuhimu wa elimu katika kupambana na umaskini na kuimarisha maendeleo ya jamii.
Makonda amempongeza Rais wa Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, akisema ujenzi wa shule na uboreshaji wa miundombinu ni hatua muhimu kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Amesema elimu ni msingi wa maendeleo, hivyo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanaenda shule na kupata fursa ya kujifunza katika mazingira salama na rafiki.
Makonda ametoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kukuza vipaji katika sanaa, utamaduni na michezo.

Amesema ushirikiano wa wazazi, walimu na Serikali ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hamduni, amesema Shule ya Msingi Butiriti imejengwa kwa gharama ya Sh milioni 330 na inatoa elimu ya awali na msingi kwa wanafunzi zaidi ya 630.
Amesema shule hiyo ina madarasa saba na imejengwa baada ya kubainika kuwa majengo ya zamani yalikuwa chakavu na hayakukidhi mahitaji ya mazingira bora ya kujifunzia.

Hamduni ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo elimu, ili kuongeza fursa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, amepongeza ujenzi wa shule hiyo, akisema utasaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.



