Makubaliano ya amani hatarini kuvunjika

SUDAN KUSINI : KUZUILIWA kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, kumetishia mkataba wa amani wa 2018, uliohitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Msafara wa maafisa wa usalama, akiwemo waziri wa ulinzi, ulivamia makazi ya Machar katika mji mkuu, Juba, na kuwatwaa silaha walinzi wake.
Machar alikamatwa pamoja na mkewe, Angelina Teny, ambaye ni waziri wa mambo ya ndani. SOMA: Mazungumzo ya amani Sudan Kusini yaanza
Naibu kiongozi wa SPLM/IO, Oyet Nathaniel Pierino, alisema kuwa tukio hili limesababisha kushindwa kwa makubaliano ya amani, na kuongeza wasiwasi kuhusu mustakabali wa amani.
Serikali ya Sudan Kusini haijatoa tamko rasmi kuhusu tukio hili. Rais Salva Kiir alieleza kukerwa kwake na tukio hilo, akisisitiza kutotaka kurejesha nchi kwenye vita.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukionya kuhusu hatari ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, kutokana na mivutano kati ya Machar na Kiir.
Ingawa walikubaliana kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Agosti 2018, uhusiano wao umekuwa ukiharibika kutokana na ghasia na mivutano ya kikabila.



