Malengo ya uchumi 2025/2026, mikakati kuongeza mapato

JUNI 12, 2025 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/2026 bungeni Dodoma ambayo ni Sh trilioni 56.49. Makala ya MWANDISHI WETU inatazama baadhi ya vipengele vikiwamo vyashabaha za uchumi jumla na mikakati ya kuongeza mapato. Fuatilia. 

Katika hotuba yake, Dk Mwigulu anawambia Watanzania kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2025/2026 Sh trilioni 56.49 imeandaliwa kwa kuzingatia mambo kadhaa muhimu ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026).

Aidha, imezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020, Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 pamoja na nyaraka, miongozo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Anabainisha: “Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/2026 ni ya tano na mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.”

Anasema: “Dhima kuu ya Bajeti ya Mwaka 2025/2026 kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni: ‘Mageuzi Jumuishi ya Uchumi Kupitia Uimarishaji wa Ukusanyaji Mapato ya Ndani, Uwekezaji wa Kimkakati wenye Kuzalisha Fursa za Ajira na Uboreshaji wa Hali ya Maisha ya Wananchi.”

Shabaha za uchumi jumla Kwa kuzingatia mwenendo wa viashiria mbalimbali vya uchumi jumla na utekelezaji wa bajeti ya serikali, Waziri wa Fedha anabainisha shabaha na malengo ya uchumi jumla kwa mwaka 2025/2026 akisema ni pamoja na hasa kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa hadi kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2024.

Mengine ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa, unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika muda wa kati, kuongeza mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 16.7 ya Pato la Taifa mwaka 2025/2026 ikilinganishwa na asilimia 15.8 mwaka 2024/2025.

Pamoja na hayo, shabaha na malengo mengine ni kuwezesha mapato ya kodi kufikia asilimia 13.3 ya Pato
la Taifa mwaka 2025/2026 kutoka asilimia 12.8 mwaka 2024/2025, kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha
misaada) kutoka asilimia 3.4 ya Pato la Taifa mwaka 2024/2025 hadi kuwa asilimia 3.0 mwaka 2025/2026 pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

“Uandaaji wa shabaha na malengo ya uchumi jumla kwa mwaka 2025/2026 umezingatia misingi inayojumuisha kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara, kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili yakiwamo ya ukame, vita, magonjwa ya mlipuko na mafuriko pamoja na uchumi imara wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa.”

Misingi mingine ni kuendelea kuimarika kwa upatikanaji na usalama wa chakula nchini pamoja na uwepo wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani.”

Maeneo ya Vipaumbele kwa Mwaka 2025/2026
Anasema bajeti hiyo inaendeleza na kukamilisha utekelezaji wa miradi, programu za maendeleo na afua zinazochangia maeneo makuu ya vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Vipaumbele hivyo kwa mujibu wa Dk Mwigulu ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara pamoja na kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu ili kuhakikisha ufikiwaji wa malengo ya Dira 2025.

Anasema: “Baadhi ya maeneo mahususi yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/2026 ni pamoja na kuendelea kutekeleza na kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati na kuimarisha sekta za uzalishaji zenye matokeo chanya katika kukuza uchumi, kuimarisha rasilimali watu hususani katika sekta za huduma za jamii pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.”

Anaongeza: “Maeneo mengine mahususi ya vipaumbele ni pamoja na ugharamiaji wa deni la serikali; mishahara na stahiki za watumishi wa umma pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027.”

Eneo lingine la kipaumbele cha bajeti ya Mwaka 2025/2026 kwa mujibu wa Mwiguluni Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Kuhusu gharama za uchaguzi huu, Dk Mwigulu anasema: “Nipende kuwafahamisha Watanzania kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 tutaugharamia kwa fedha zetu za ndani… Nitumie fursa hii kulihakikishia Bunge kuwa, Serikali imejipanga na itahakikisha upatikanaji wa fedha kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati.”

Kimsingi, hili ni jambo la kujivunia na kuwapongeza Watanzania na Serikali yao. Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya waziri wa fedha, maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 hususani katika kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi.

Ni kwa msingi huo Mwigulu anawambia Watanzania: “Ninawasihi na kuwaomba wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kukichagua kwa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025. Hakika mwaka 2025 Watanzania tunaenda na Mama.”

Mikakati ya kuongeza mapato
Katika Aya ya 135 ya Bajeti hiyo, serikali inasema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Ikumbukwe kuwa upatikanaji wa mapato yakiwa yatokanayo na kodi ndio msingi na kichocheo kikuu cha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii Pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Mwigulu, hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato zinazokusudiwa na serikali ni pamoja na kuendelea kuhamasisha umma kuhusu kutoa na kudai risiti za malipo za kielektroniki (EFD) na kuboresha utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vinavyosimamiwa na mamlaka za udhibiti.

Hatua nyingine Dk Mwigulu anasema ni “Kuendelea kuboresha Mfumo wa TAUSI ili kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa vinajumuishwa katika mfumo huo pamoja kuongeza ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya mashirika, taasisi za umma na wakala za Serikali ili kuhakikisha gawio na michango stahiki inawasilishwa kwa wakati.”

Aidha, hatua nyingine anasema ni kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) na kuendelea kuhamasisha matumizi ya njia za kidijiti katika kufanya malipo wakati wa ununuzi wa bidhaa na huduma.

Kwa niaba ya serikali, Waziri wa Fedha anasema mikakati ya usimamizi wa matumizi katika mwaka 2025/2026 itajumuisha kuendelea kusimamia na kuimarisha matumizi sahihi ya mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika utekelezaji wa shughuli za serikali ikijumuisha mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu, malipo serikalini, ununuzi na usimamizi wa mali za serikali.

Mikakati mingine ni kuimarisha uwajibikaji na udhibiti katika matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuziba mianya ya ubadhirifu kwa lengo la kupata thamani ya fedha katika matumizi ya Serikali na kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kuokoa gharama za ziada zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button