‘Mali ziuzwe kufidia waliopigana Vita ya Dunia’

DODOMA; ASKARI waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia walikuwa 737, kati yao 57 wapo hai na 680 wamefariki, Bunge limeelezwa.
Pia Bunge limeelezwa kuwa Kamati maalum iliyoundwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imetoa mapendekezo ya kuuza mali zisizo na utata za Shilingi 15,952,574,800 na kutoa fidia kwa maveterani wote (walio hai, na warithi wa waliokwishafariki) na kuwapatia bima ya afya maveterani walio hai waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha, Sylivestre Koka, aliyetaka kujua kuna mkakati gani kuhakikisha wazee waliopigana Vita ya Pili ya Dunia chini ya Chama cha TLC wananufaika na mali zao.
Akijibu swali hilo Waziri Tax amesema kufuatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 18, 2022, wizara iliunda kamati maalum kuchambua na kutoa ushauri kuhusu hatima ya askari waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia (Maveterani) mwaka 1939 – 1945, na kuhusu mali za chama cha Tanzania Legion & Clubs (TLC).
“Tathmini iliyofanywa na kamati, ilibaini kuwa askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia walikuwa 737, kati yao 57 wapo hai, na 680 wamekwishafariki. Tathmini ilionesha pia kuwa TLC, inazo mali zenye thamani ya Shilingi 37,366,323,048.000.
“Hata hivyo, baadhi ya mali hizo zina madeni, na zingine zipo chini ya usimamizi au umiliki wa taasisi nyingine, na hivyo kusababisha mashaka kuhusu umiliki wake.
“Katika hali hii, mali zilizothibitishwa kuwa za TLC bila utata zina thamani ya Shilingi 15,952,574,800. Tathmini ilionesha pia kuwa, maveterani walio hai wanahitaji matunzo ikiwa ni pamoja, na bima ya afya.
“Mheshimiwa Spika, Kamati imetoa mapendekezo ya kuuza mali zisizo na utata za Shilingi 15,1952,574,800 na kutoa fidia kwa Maveterani wote (walio hai, na warithi wa waliokwisha fariki); kuwapatia bima ya afya Maveterani walio hai; na kuwaenzi maveterani wote kwa kujenga mnara wa kumbukumbu wa askari wote waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
“Serikali inafanyia kazi mapendekezo haya, na tathmini kuhusu mali zenye utata inaendelea,” amesema Waziri Tax.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button