WATAALAM wa mabadiliko ya tabianchi na uchumi wamebainisha mambo saba yatakayosaidia kukabiliana na hali ya kushuka kwa pato la taifa kutokana na athari ya mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuonekana nchini.
Katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) Rais Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inapoteza asilimia mbili hadi tatu kutokana na mabadiliko hayo.
Wakizungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti wataalamu hao wamesema kuna haja ya kutumia rasilimali zilizopo kukabilina na mabadiliko hayo.
Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi na Jamii ,Oscar Mkude amesema hatua ya kwanza ni kuacha au kupunguza viwango vya uharibifu wa mazingira kwa kurudisha uoto wa asili ikiwemo kupanda miti aina ya mikoko ambayo inauwezo mkubwa wa kupunguza hewa chafu.
“Mikoko ni mizuri kupunguza hewa ukaa kwani mkoko mmoja unapunguza hewa ukaa mara nne ya mti wa kawaida,Mwambao wa pwani kulikuwa na mikoko mingi imepotea na inaota ndani ya muda mfupi tu miaka mitatu au minne ni sehemu ya kurudisha uoto wa asili,”alisema.
Hatua ya pili amesema ni muhimu kulima kilimo ambacho kinaendana na alama ya wakati ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kutokana na kubadilika kwa misimu.
“Misimu sasa imebadilika kuna maeneo mvua zimepungua na kuna maeneo mvua zimeongezeka na tunahitaji mvua za kiasi na wakati na mvua hazipo katika wakati kwasababu ya mabadiliko hiyo imefanya uzalishaji kupungua na kama uzalishaji umepungua hata pato la taifa litaathirika na uchumi wetu unategemea kilimo kwa kiasia kikubwa.
Mkude amesema Mbinu ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji inahitaji maeneo yanayaofaa kujengwa miundombinu maji ya umwagiliaji na wakulima walime na kupata tija badala ya kusubiri mvua.
Kuhusu ukuaji wa viwanda Mkude ameeleza kuwa Tanzania bado ipo katika hatua ya kukua hivyo inatakiwa kutumia nishati ambayo haina hewa ukaa kuanzia sasa ili baadae isirudi tena nyuma kwani sasa uzalishaji ni mdogo lakini baada ya miaka ijao utaongezeka hivyo muhimu kujikita katika nishati safi.
Amebainisha kuwa ni muhimu kupunguza utegemezi wa hali ya hewa kama miundombinu ya umeme inayotumia maji kwani kama hali za mvua haieleweki italeta usumbufu.
“Uchumi wa nchi unakua na watu wanaongezeka miaka 50 ijayo hata Bwawa la Nyerere halitoshi na mvua hazitatosha tunahitaji pia umeme wa jua na upepo kwani upo na bado hatujatumia,Vyanzo vya maji sio vya kuaminika kwa miaka ijayo kutokana na mabadiliko tutumie maarifa kujikinga na kujihami.
Amefafanua kuwa mataifa makubwa yanawajibu wa kusaidia nchi zinazoendelea kwasababu maumivu yaliyopo leo wanasababisha wao kutokana na kuzalisha hewa chafu kwa miaka mingi na tunaathirika wote na Dunia itakuwa mbaya.
Kwa upande wake Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Israel Sostenes amesema ni muhimu kuangalia sheria zilizopo na kama zinamapungufu kuna haja ya kufanya marekebisho ili kudhibiti uharibifu huo ikiwepo watu kuelimishwa au uwezeshaji wa fedha na vitendea kazi ili washiriki kuhifadhi mazingira.
Aidha amesema ni wakati wa nchi sasa kutumia madini yaliyopo ya kuzalisha nishati safi kwa kuuza nje ya nchi na kujipatia faida kubwa na pia kutumia madini hayo kuzalisha nishati safi ndani ya nchi.
“Kwasasa tunakoelekea madini yanayotumika kuzalisha nishati safi yatahitaji zaidi Duniani ni muda wa kupata fedha nyingi kutoka kwa madini hayo na pia yatumike ndani ya nchi kama fursa za mabadiliko ya tabianchi,alisisitiza.
Habari hii imewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.