Mambo makubwa yaja miaka 60 Hifadhi ya Ruaha
IRINGA; Makundi mbalimbali ya kijamii yanatarajia kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
Sherehe hizi zitafanyika kwa wiki moja, kuanzia Oktoba Mosi hadi 10, mwaka huu, zikitumika kutangaza mafanikio, fursa, na mchango wa hifadhi hiyo katika kukuza utalii na uhifadhi nchini.
Mkuu wa hifadhi hiyo, Godwell Ole Meing’ataki, alieleza kuwa Hifadhi ya Ruaha ni mojawapo ya maeneo muhimu ya uhifadhi nchini Tanzania, na imepiga hatua kubwa katika kulinda wanyamapori na kuimarisha utalii.
Akizungumzia ukubwa na uzuri wa hifadhi hiyo, Meing’ataki alisema Ruaha ni makazi ya tembo zaidi ya 15,000, nyati zaidi ya 20,000, na simba zaidi ya 800 wanaotembea kwa makundi makundi jambo linaloongeza ladha ya utalii.
Isome pia: Mpaka Hifadhi ya Ruaha warekebishwa
“Hifadhi hii pia ni maarufu kwa wanyama kama kudu wakubwa na wadogo, pofu, swala pala, chui, mbweha, fisi na mbwa mwitu, na Mto Ruaha Mkuu wenye samaki, viboko, na mamba kwa wingi,” amesema.
Amesema Hifadhi ya Ruaha ni paradiso ya utalii wa ndege, ikiwa na zaidi ya aina 500 za ndege, wakiwemo wanaohama kutoka kaskazini na kusini na mimea inayopatikana katika hifadhi hiyo inawakilisha karibu aina zote za mimea ya Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Meing’ataki amesema takwimu hizo zinaonesha mafanikio makubwa katika uhifadhi, jambo ambalo limechochea ongezeko la utalii na watalii na kuchangia pato la taifa.
Amesema katika maadhimisho hayo, makundi mbalimbali yatashiriki ziara zinazoangazia historia na utajiri wa Ruaha.
“Ziara ya siku ya kwanza itaongozwa na machifu na wazee wa kimila, ambapo watapata taarifa za uhifadhi. Siku ya pili itakuwa kwa viongozi wa dini na kamati ya amani ya mkoa, pamoja na walemavu,” amefafanua.
Pia amesema, maadhimisho hayo yataambatana na utoaji wa misaada katika vijiji vinavyozunguka hifadhi na kongamano la miaka 60 litakalojadili mafanikio na changamoto za hifadhi hiyo.
“Tutakuwa pia na michezo na burudani katika kijiji cha Tungamalenga, na ziara ya wawekezaji kwa ajili ya kutathmini fursa za uwekezaji katika hifadhi,” alisema Meing’ataki, akiongeza kuwa mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana.