Mambo yameiva Tanzania Fashion Festival

DAR ES SALAAM: Jukwaa la ubunifu wa mavazi nchini maarufu kama Tanzania Fashion Festival, msimu wa saba litafanyika Septemba 26, 2026 likinogeshwa na Video Queen, Fayvanny Ukumbi wa Terrace Slipway, ijini Dar es Salaam.
Msemaji wa tamasha hilo, Bhoke Egina, amesema kila msimu umekuwa na utofauti wake, huku mwaka huu wakitarajia kumpokea Fayvanny kama mgeni rasmi.
Amesema pia jukwaa hilo litawakutanisha warembo mbalimbali, akiwemo Miss Grand Tanzania, Beatrice Alex na Miss Grand Kilimanjaro, Tess Kessy.
“Kila msimu tunakuwa na utofauti. Mwaka huu tumepata muitikio mkubwa kutoka kwa warembo, hivyo tumeamua kuwapa nafasi zaidi kushiriki katika jukwaa hili,” amesema
Amesema Tanzania Fashion Festival inalenga kukuza sanaa za maonesho, kuibua vipaji vipya na kuwapa nafasi wabunifu wachanga kuonyesha kazi zao bila gharama.

“Lengo la jukwaa hili ni kuendeleza na kukuza sanaa za maonesho, kuibua na kuunga mkono vipaji vipya vinavyochipukia. Mbunifu anatakiwa kuandaa mavazi yake na kuja kuyaonesha katika jukwaa hili bila gharama,” amesema.
Amesema tamasha hilo litawakutanisha mastaa mbalimbali kutoka katika tasnia ya muziki wa bongo fleva, filamu, mitindo na sanaa nyingine za maonyesho, pamoja na viongozi na wadau wa tasnia.
Amesema aliamua kuanzisha jukwaa hilo kutokana na kutambua mchango wake katika tasnia ya ubunifu wa mavazi na kutaka kuwainua wabunifu wachanga.
“Kwa kutambua mchango wangu katika tasnia ya ubunifu wa mavazi nchini, niliamua kuandaa jukwaa hili ili kuibua wabunifu wachanga na kuzidi kuipa nafasi tasnia ya mavazi nchini,” amesema.



