WATU watano wanaodaiwa kuwa ni matapeli na kufanikiwa kuchota mamilioni ya pesa kwa kujifanya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) wakekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha katika maeneo tofauti tofauti mkoani hapa.
Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP, Justine Masejo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Fredy Malaki (34) mkazi wa Karakata, Francis Mwita (42) mkazi wa Ukonga, Fidelis Joseph (27) mkazi wa Msumi Mbezi, Selina Fortunatus (43) makazi wa Temeke wote kutoka Jijini Dar es salaam na Fereji Hamadi (40) mkazi wa Tabora.
Aidha ACP Masejo amebainisha kuwa bado jesho hilo linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapo kamilika jalada litapelekwa ofisi ya taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo, ACP Masejo ametoa wito kwa wananchi kujiridhisha na watu wanaofika maeneo yao ya biashara na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA ambapo amewaomba wananchi kutoa taarifa za baadhi ya watu hao wachache wanaofanya matukio ya uhalifu hususani ya utapeli katika mkoa huo ili hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake Ofisa wa kodi mwandamizi kutoka mamlaka hiyo, Hamenyimana Ayoub amesema TRA imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa Wananchi kuhusiana na uwepo wa baadhi ya watu wanaojiita maafisa wa mamlaka hiyo na kuchukua fedha kwa Wànanchi.
Ofisa huyo mwandamizi amendelea kufafanua kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo alitoa taarifa kwa Polisi ndipo kwa kushirikiana na jeshi hilo pamoja na Wananchi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao huko maeneo ya Manyara Kibaoni Wilayani Karatu wakati wakijaribu kutoroka.
Naye Karatu John ambaye ni muhanga amebainisha kuwa watuhumiwa hao walifika dukani kwake na kujitambulisha kuwa ni maafisa wa TRA na kuanza kuwahoji huku wakitaka kulipwa kiasi cha fedha ya kitanzania Milioni nne na nusu.