ILI jamii iwe na ustawi bora inahitaji afya njema ya kimwili na akili kumrahisishia mtu kufanya kazi zake akiwa na utimamu.
Ustawi mzuri huleta amani na furaha na amani huleta maendeleo mazuri kati ya jamii husika.
Na uwepo wa huduma za ustawi wa jamii ni muhimu zaidi kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii ikiwemo masuala ya ushauri wa kisaikolojia.
Ili kufanikisha huduma nzuri ya ustawi za wa jamii Chuo Kikuu cha Agder kilichopo nchini Norway kwa kushirikiana na Taasisi za Ustawi wa Jamii Tanzania, Rwanda na Uganda wameanzisha mradi maalumu wa kuwapa mafunzo na kuwasogeza karibu na wananchi maofisa ustawi wa jamii zaidi ya 30.
Mradi huo pia unalenga kujenga uelewa kwa maofisa ustawi wa jamii na kujua mambo katika jamii zao kueneza elimu ya ustawi wa jamii zaidi.
Akizungumza na HabariLEO katika mahojiano maalumu, Kiongozi wa Mradi huo kutoka Chuo cha Agder, Profesa Ann Nilsen, anasema mradi huo unahusisha kuonesha waathirika, utafiti na kuwajengea uwezo wa elimu ya kuwa karibu na jamii.
“Tunajifunza zaidi jinsi ya kufanya kazi ndani ya jamii husika kujenga uelewa unaoendana na wao, tutahusisha majadiliano kuhusu kazi za ustawi wa jamii, baada ya mradi natarajia maofisa hawa wa jamii wataenda kufanyia kazi vitu tulivyowafundisha na pia watawafundisha wengine katika vyuo na jamii,” anaeleza Nilsen.
TAFITI
Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Mratibu wa mradi huo Tanzania, Dk Zena Mabeyo anasema katika mradi huo taasisi imeanza kufaidi kwani wanafunzi watatu kwa ngazi ya shahada ya uzamivu katika fani ya ustawi wa jamii ambao pia ni wahadhiri wasaidizi wa taasisi hiyo, wamesomeshwa.
“Taasisi mwaka huu imepanga na kutekeleza mradi kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanne kwa ngazi ya shahada ya uzamili katika fani hiyo na tunapanga kusomesha wengine sita kuanzia mwaka huu wa masomo katika ngazi hiyo.
Anabainisha kuwa taasisi kupitia mradi imetekeleza ujenzi wa maabara ya jamii na wanafunzi 12 walipelekwa katika mikoa mitatu ya Iringa, Mtwara na Tanga ili wakafanye kazi katika jamii kusaidia jamii hususani wazee kuelewa matatizo yao.
“Sio hilo tu pia kuangalia fursa zao na kushirikiana nao katika kubuni miradi ya maendeleo, tunategemea mpaka kumalizika mradi tutakuwa tunawalipia wanafunzi 36 kwenda kuishi na jamii, kufanya kazi na jamii na kutatua changamoto zinazowakabili wazee,” anasisitiza Dk Mabeyo.
Anasema wamefanya pia ushirikiano katika kufundisha na kuandaa semina za mtandaoni zinazotoa miongozo na mafunzo ya jamii.
Dk Mabeyo anasema lengo ni kujenga jamii jumuishi kupitia uwezeshaji katika elimu katika kazi kwa vitendo. Mradi huo ni wa miaka sita (2020-2026).
“Baada ya mradi huu tutakuwa tumetoa ufadhili kwa wanafunzi 10 ambao ni familia zisizojiweza kupata elimu wa shahada ya uzamili,” anasema Dk Mabeyo.
Anasema watakuwa wamechangia jitihada za serikali kuondoa umasikini na kuimarisha maisha katika ngazi ya familia hususani kundi la wazee.
WANAFUNZI WAELEZA WATAKAVYONUFAIKA
Mwanafunzi anayenufaika na mradi huo kutoka Tanzania, Frank Gasper anaeleza mradi huo ni nafasi ya kukua kitaaluma na kuongeza maarifa na wameshirikiana na nchi nne.
“Nikimaliza ni muda wa kurudisha kwa jamii nilichokipata hapa ukizingatia katika kada hii ni kujenga jamii inayoweza kugusa watu. Mfano hapa Tanzania tunaweza kugusa wazee kwa mikoa mitatu tutazidi kuangalia namna gani ya kuboresha na kujifunza lakini pia kuendeleza kazi ya ustawi wa jamii,” anasema Gasper.
Mwanafunzi kutoka Rwanda, Pierre Meimara, anasema anapata mafunzo ya shahada ya uzamivu ya ustawi wa jamii na nafasi hiyo ni nzuri.
“Kwa sababu nimelenga kusomea hii muda mrefu na itanijenga na pia najihusisha na kupinga ukatili kwa watoto, itanisaidia kuleta matokeo mazuri katika jamii kwa tafiti mbalimbali na nitafanya kazi kwa bidii,” anasema Pierre.
MPANGO WA SERIKALI
Mpango wa serikali ni kupeleka maofisa ustawi wa jamii katika ngazi zote nchini kuanzia kata hadi taifa kufanikisha huduma hizo kuwa karibu zaidi na wananchi kwani zinahitajika kwa kiasi kikubwa kulingana na changamoto zilizopo katika jamii.
Serikali imedhamiria kuimarisha utoaji huduma za ustawi wa jamii katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii ya Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, anasema uamuzi huo wa serikali umewekwa baada ya mkuu wa chuo kutoa taarifa namna ambavyo chuo hicho kinatoa huduma za ushauri na jinsi kinavyoshirikiana na jamii kutatua changamoto zinazoikabili.
Mpanju anasema chuo hicho kinafanikisha huduma ya elimu na msaada wa kisaikolojia kwa wananchi, mashirika na taasisi binafsi na za serikali.
“Kazi mnayoifanya ni nzuri na kubwa, nilichopenda zaidi ni vile mlivyobadilika na kukidhi mahitaji ya vijana kwa sababu mlikuwa kitaaluma zaidi lakini sasa mmekuwa na programu ya ushiriki jamii. Hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi hii katika kutatua changamoto za kijamii,” anasema Mpanju.
Aidha, Mpanju anasisitiza uboreshaji wa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ndani ya chuo hicho huku akitoa ahadi ya serikali yakupeleka wataalamu wa lugha ya alama kutoka wizarani.
Naibu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Baraka Makona anasema atasimamia utekelezaji wa yote waliyokubaliana kati ya wizara na menejimenti ya chuo kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za taasisi.
“Tunataka taasisi hii kwa misingi ya mahitaji kama vile kuchapisha vitabu vya wasioona kuwepo na mashine hapa ambayo tutakuwa tunatumia,” anasema Makona.
Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni anatoa shukrani na pongezi kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya taasisi pamoja na kuwapatia kibali cha kuajiri watumishi wapya 52 ambao wataongeza ufanisi katika kufundisha.