Maonesho Tanzanite Kwaraa yafungua fursa masoko

MANYARA: WAFANYABIASHARA mkoani Manyara wamepata fursa ya kujifunza mbinu za kupanua masoko, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano ya kibiashara kupitia Maonesho ya Nne ya Biashara ya Tanzanite Kwaraa yanayofanyika wilayani Babati.

Maonesho hayo yanawakutanisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali, yakitoa nafasi ya kujifunza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika uzalishaji, utangazaji na uuzaji wa bidhaa ili kuongeza tija na kuwafikia wateja wengi zaidi.

Meneja Masoko wa kampuni ya Mati Super Brands Ltd., Isack Piganio, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara kupanua mitandao yao ya kibiashara na kutafuta masoko mapya, hatua inayoweza kusaidia kukuza shughuli zao na kuchangia maendeleo ya uchumi.

“Ushiriki wetu unalenga kupanua soko la bidhaa za kampuni pamoja na kuwapa wafanyabiashara na wadau fursa ya kujenga mahusiano ya kibiashara na kutafuta masoko mapya,” amesema Piganio.

Ameipongeza Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), Mkoa wa Manyara, kwa kuandaa maonesho hayo yanayotoa nafasi kwa wafanyabiashara kukutana, kujifunza na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuboresha shughuli zao.

Amesema matumizi ya teknolojia na ubunifu yanaweza kuwasaidia wafanyabiashara kuongeza ushindani na kupanua wigo wa masoko, ikiwemo kutumia mifumo ya kidijitali kutangaza bidhaa na kuwafikia wateja.

Maonesho ya Tanzanite Kwaraa ni mojawapo ya majukwaa yanayoweza kuwaunganisha wafanyabiashara na wateja, kukuza uelewa wa fursa za biashara na kuhamasisha ushirikiano unaoweza kuchangia maendeleo ya uchumi wa jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button