Mapambano dawa za kulevya yanahitaji mshikamano wa kitaifa
KILA Juni 26, dunia huadhimisha Siku ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya, ikiwa ni jitihada za kuhamasisha jamii na mataifa kuwa na msimamo thabiti dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Hapa nchini, maadhimisho haya yanafanyika leo mkoani Dodoma. Dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa ustawi wa jamii, afya na maendeleo ya kiuchumi.
Athari zake ni kubwa kwani husababisha uharibifu wa afya ya watu, huchangia uhalifu, zinavuruga maendeleo ya kijamii.
Watumiaji wa dawa za kulevya mara nyingi hupoteza maadili, kushindwa kufanya kazi na hata kuhatarisha maisha yao na ya wengine.
Tunatambua jitihada za Serikali ya Tanzania katika kupambana na janga hili kwa njia mbalimbali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Hatua madhubuti zimekuwa zikichukuliwa kukabiliana na biashara hii haramu. Mfano mzuri ni pamoja na operesheni za mara kwa mara dhidi ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo.
Aidha, serikali imeimarisha sheria zinazodhibiti matumizi ya dawa zinazokubalika na kuimarisha usimamizi wa vituo vya matibabu kwa lengo la kuwasaidia watu walioathirika na dawa za kulevya kujiondoa kwenye ulevi huo hatarishi.
Hata hivyo, jitihada hizi pekee hazitoshi. Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa karibu baina ya serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla.
Ni muhimu kuimarisha elimu na uhamasishaji kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa vijana na jamii kwa ujumla ili kuwazuia kujihusisha na matumizi yake.
Viongozi wa dini, walimu shuleni na vyuo, na wazazi wanapaswa kuwaongoza vijana kuwa mfano mzuri kwa vijana, kuwahamasisha kuishi kwa maadili mema na kujiepusha na matumizi ya dawa hizo hatarishi.
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja wetu. Kuendelea kuhimiza usalama, afya, na maendeleo ya jamii kunahitaji juhudi za pamoja na msukumo wa hali na mali.
Tunaipa heko serikali kwa hatua mbalimbali inazofanya huku tukihimiza iendelee kuimarisha sheria, kuboresha mifumo ya usimamizi, na kuanzisha kampeni za elimu za mara kwa mara.
Mikakati endelevu iwekwe ikizingatia mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia, na ivutie makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kuathirika na biashara hii yaelewe na kuiunga mkono ili kuwaepusha ama kujihusisha na biashara au matumizi ya dawa hizo.
Rai yetu ni kwamba, panahitajika mshikamano wa kitaifa kwa maana ya kila mmoja kuwa sehemu ya mikakati ya kukabili biashara na matumizi ya dawa hizo kwa ustawi wa nchi.
Kila mwananchi kwa nafasi yake anapaswa kushikamana, kuimarisha juhudi za pamoja na kuhakikisha kwamba jamii inakuwa salama, yenye afya, na yenye maendeleo endelevu.
Maadhimisho ya leo ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya yaendeleze wito kwa jamii kutoiachia serikali pekee bali mapambano yawe ya kila mmoja.



