Marekani kusitisha misaada ya kijeshi Ukraine

WASHINGTON DC: RAIS wa Marekani, Donald Trump, ameagiza kusitishwa kwa misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mvutano wake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy uliotokea wiki iliyopita kwa mujibu wa afisa mmoja wa Ikulu ya White House.
“Rais Trump amekuwa wazi kuhusu azma yake ya kutafuta amani. Tunataka pia kuona washirika wetu wakijitolea kwa lengo hilo. Hivyo, tunasitisha misaada yetu na kuikagua ili kuhakikisha inachangia katika suluhisho la kudumu,” amesema ofisa huyo wakati akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
Uamuzi huu unafuatia mabadiliko ya sera za Marekani kuhusu Ukraine na Urusi tangu Trump alipoingia madarakani Januari mwaka huu, ambapo ameonyesha msimamo wa kirafiki zaidi kwa Moscow.
Hatua hiyo imechochewa zaidi na mabishano makali kati ya Trump na Zelenskiy siku ya Ijumaa katika Ikulu ya White House, ambapo Trump alimshutumu kiongozi huyo wa Ukraine kwa kutokuwa na shukrani ya kutosha kwa msaada wa Washington katika vita dhidi ya Urusi.
Chanzo: Reuters


