Marekani Yaendeleza Diplomasia Asia

MALAYSIA:WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amehitimisha siku yake ya pili na ya mwisho katika mkutano wa usalama wa Jukwaa la Kikanda la Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) uliofanyika nchini Malaysia.
Katika ziara hiyo, Rubio alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, wakati ambapo mvutano kati ya Marekani na China unaendelea kuongezeka kuhusu masuala ya biashara, usalama wa kikanda, pamoja na msimamo wa China kuhusu vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Mkutano huo ulifanyika muda mfupi baada ya Rubio kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambapo walijadili kuhusu njia mbadala za kuanzisha mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine.
Ziara ya Rubio imekuja katika kipindi ambacho kuna wasiwasi mkubwa wa kimataifa na kikanda kuhusu mwelekeo wa sera za Marekani, hususan katika nyanja za biashara, usalama na diplomasia. SOMA: Harvard yabanwa na Marekani, China yakerwa
Hii ni kufuatia matamko ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu uwezekano wa kuanzisha ushuru mkubwa kwa baadhi ya washirika na hata mahasimu wa kiuchumi wa Marekani.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema kuwa mikutano ya aina hii ni muhimu katika kujenga majadiliano ya kidiplomasia, hasa ikizingatiwa kuwa eneo la Asia ya Kusini Mashariki linazidi kuwa muhimu katika mahusiano ya kimataifa kutokana na nafasi yake ya kiuchumi na kijeshi.