Harvard yabanwa na Marekani, China yakerwa

WASHINGTON : SERIKALI ya China imeikosoa vikali hatua ya Marekani ya kukifutia Chuo Kikuu cha Harvard haki ya kuandikisha wanafunzi wa kigeni, wengi wao wakiwa raia wa China, ikieleza kuwa uamuzi huo unahatarisha sura ya kimataifa ya Marekani katika elimu ya juu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, amesema kuwa uamuzi huo wa utawala wa Rais Donald Trump si tu kwamba ni wa kibaguzi, bali pia unaathiri mahusiano ya kielimu na kiutamaduni kati ya nchi hizo mbili.

“Hatua hii ni mwendelezo wa mashinikizo dhidi ya raia wa China na taasisi za elimu. Inatia doa dhamira ya Marekani katika kutetea uhuru wa kitaaluma na elimu ya kimataifa,” alisema Mao Ning.

Kwa upande wake, uongozi wa Chuo Kikuu cha Harvard, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, umeeleza masikitiko yake na kusema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mashambulizi ya serikali ya Marekani dhidi ya mfumo wa elimu ya juu, hasa katika taasisi zinazopokea wanafunzi wa kimataifa.

Takwimu za hivi karibuni kutoka Harvard zinaonesha kuwa wanafunzi 6,700, sawa na asilimia 27 ya jumla ya wanafunzi, wanatoka nje ya Marekani, wengi wao wakiwa kutoka China na India.

Chuo hicho maarufu duniani kimewahi kutoa mafunzo kwa washindi 162 wa Tuzo ya Nobel, na kimekuwa nguzo muhimu ya ushirikiano wa kielimu kati ya Marekani na mataifa mengine.

Wachambuzi wa mambo ya kimataifa wanasema hatua hiyo inaweza kudhoofisha mvuto wa Marekani kama kitovu cha elimu ya juu duniani, na kuongeza mivutano ya kidiplomasia kati ya Washington na Beijing.

SOMA: Marekani: Vifaa vya simu,elekroniki vyapandishwa ushuru

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button