GAZA, Palestina – Marekani imesitisha mpango wa kupeleka shehena ya silaha kwa Israel, katika hali inayoonyesha kupinga uamuzi wa Israel kuvamia mji wa Rafah kusini mwa Gaza, ambapo mamia ya maelfu ya Wapalestina wanaokimbia vita wametafuta hifadhi.
Afisa wa Marekani, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alidai kwamba wakati viongozi wa Israel walionekana kukaribia uamuzi juu ya shambulio hilo, utawala wa Joe Biden “ulianza kupitia kwa makini mapendekezo ya uhamisho wa silaha fulani kwenda Israeli ambazo zinaweza kutumika Rafah”, kuanzia mwezi Aprili.”
“Kutokana na ukaguzi huo, tumesitisha shehena moja ya silaha wiki iliyopita,” afisa huyo alisema.
Wakati huo huo, afisa wa Hamas aitwaye Osama Hamda alionya kwamba ikiwa uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Rafah utaendelea, hakutakuwa na makubaliano ya mapatano.
Marekani, hata hivyo, ilieleza matumaini yake kwamba tofauti zilizosalia kati ya Israel na Hamas zinaweza kutatuliwa katika meza ya mazungumzo kuhusu pendekezo la hivi karibuni la kundi la wanamgambo wa Kipalestina la kusitisha mapigano huku mazungumzo yakiendelea mjini Cairo leo.
Wanajeshi wa Israel siku ya Jumanne walikamata kivuko kikuu cha mpaka kati ya Gaza na Misri huko Rafah, na kukata njia muhimu ya msaada katika eneo ndogo la Palestina.