Mtandao bila ukatili inawezekana

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam H. Mwinyi, ametoa wito kwa jamii kushirikiana kutokomeza ukatili wa kijinsia mtandaoni, akisema ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja.
Akizungumza katika kongamano la Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia lililoandaliwa na TAWJA – Zanzibar, Mama Mariam amesema pamoja na fursa za kidijitali, kumekuwa na ongezeko la vitendo vya matusi, vitisho na usambazaji wa taarifa binafsi bila ridhaa, vinavyowaathiri zaidi wanawake na wasichana.

Amesisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana, wazazi, walimu na jamii kuhusu usalama mtandaoni, sambamba na kuimarisha mifumo ya kisheria na utoaji wa huduma kwa waathirika, ikiwemo ushauri wa kisaikolojia. SOMA: Mariamu Mwinyi kuhudhuria OAFLAD
Kupitia ZMBF, Mama Mariam amesema zaidi ya wanufaika 3,600 wamepatiwa elimu na msaada mbalimbali, huku taasisi hiyo ikishirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuandaa mfumo wa kidijitali wa kuratibu taarifa za udhalilishaji.

Ameipongeza TAWJA – Zanzibar kwa mchango wao katika kukuza haki na usawa wa kijinsia, akibainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “Tuungane Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia Mitandaoni,” inahitaji uwajibikaji na matumizi ya lugha yenye staha mtandaoni.



