Marufuku bodaboda kuingilia misafara ya viongozi

KIGOMA: POLISI Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kigoma imekemea tabia ya waendesha pikipiki zinazobeba abiria maarufu ‘bodaboda’ kuendesha pikipiki zao kwa kasi na kuingilia misafara ya viongozi na wakati mwingine kuwa mbele ya misafara hiyo.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kigoma, Ibrahim Mbaruku ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja baina ya madereva pikipiki, bajaji na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kigoma mkutano uliokuwa ukitoa elimu na ufafanuzi wa sheria mpya ya kodi ya mapato ambayo  waendesha pikipiki hao wataanza kulipa.

Mbaruku amesema kuwa boda boda hao wamekuwa wakiingilia misafara ya mawaziri, Mkuu wa mkoa na misafara mingine ya viongozi huku wakiwa hawachukuia hatua zozote za tahadhari kujiepusha na kuwaepusha watumiaji wengine wa barabara na ajali ambazo zinaweza kutokea.

Advertisement

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa polisi imeidhatiti kuhakikisha inawashughulikia boda boda wasiofuata sheria na taratibu za usalama barabarani ikiwemo pia tabia ya kubeba mishikaki, kutovaa helmet, kung’oa vioo vya pembeni ‘side mirror’ na kuweka majina yao kwenye namba ya usajili bila kufuata taratibu.