Marufuku mikataba kusainiwa bila ofisi ya AG – Rais Samia

RAIS, Samia Suluhu Hassan amepiga marufuku Taasisi za serikali kuingia mikataba bila kushirikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rais Samia amesema hayo leo Alhamisi ya Septemba 29, 2022 akifungua mkutano wa kuanzishwa chama cha kitaaluma cha mawakili wa Serikali jijini Dodoma.

Amesema siku za nyuma mikataba ilisainiwa bila ofisi ya AG kufahamu na serikali kuingia hasara kubwa, wanapopata tatizo ndio wanaikumbuka ofisi hiyo huku waliosaini wamestaafu au wametangulia mbele ya haki hivyo hakuna wa kumuuliza.

Aidha, amesema mawakili wa serikali ‘jeshi kubwa’ linalotakiwa kulinda uchumi wa Tanzania kwa kutumiia kalamu zao.

“Nyinyi ni walinzi wa kalamu na siyo walinzi wa bunduki. Ni walinzi wa kalamu na sheria zenu. Kwa hiyo mwende mkalinde uchumi wetu, kwa haki na uadilifu ili nchi hii, iweze kupokea wawekezaji wengi zaidi, tuwekeze zaidi, tukuze uchumi masilahi yapatikane.”Amesema Rais Samia na kuongeza

“Nyinyi ndio ‘majeshi wa kulinda uchumi wetu, kisheria uchumi wetu lazima ulindwe, uwekezaji lazima ulindwe, biashara lazima zilindwe na walinzi wa hayo ni nyinyi.”Amesisitiza

Amesema mawakili hao wakashughulikie kwa haki na haraka kesi za uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

“Tumefungua nchi kwa kiasi kikubwa, wawekezaji wanaingia ndani ya nchi yetu kwa kiasi kikubwa, lazima kutakuwa na vita ya kiuchumi, kutakuwa na migogoro ya kibiashara, migogoro inayokinzana na sheria zetu za uwekezaji.

“Ili tuendelee na uwekezaji mzuri na mkubwa utakaokuza uchumi wetu, lazima mawakili wa Serikali tuwe makini sana kuharakisha kusikiliza migogoro hii.

“Tukilinda uwekezaji unaowekezwa Tanzania tutakwenda kupanua wigo mpana unaokuza uchumi, wigo mpana wa kukusanya mapato na yale mliolalamikia hapa itakuwa rahisi Serikali kuyatimiza kwenu,” amsema Rais Samia huku akihaidi atawapa fungu waliloomba ili kulinda uwekezaji na kukuza uchumi.

Habari Zifananazo

Back to top button