Masauni, jeshi la polisi wajadili amani
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amefanya kikao maalumu na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi nchini kujadili usalama na amani ya nchi.
Kikao hicho, kilichofanyika jijini Dodoma, kililenga kujadili na kutathmini matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini pamoja na hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi kuzuia na kudhibiti uhalifu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Maduhu Kazi.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi, viongozi walioshiriki ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura, Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu, Suzan Kaganda, Kamishna wa Fedha na Lojistiki, Liberatus Sabas, na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Juma Haji.
Pia walikuwepo Kamishna wa Sayansi ya Uchunguzi wa Jinai, Shabani Hiki, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna Ramadhani Kingai, na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna David Misime.
Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa kuimarisha mikakati ya kuendeleza amani na usalama nchini, huku hatua za haraka za kudhibiti uhalifu zikiwa ni kipaumbele.