Mashahidi 24 kufunguka kesi ya shambulizi mgodini

MASHAHIDI 24 wanatarajiwa kutoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo 11 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kwenye kesi ya shambulizi la kudhuru mwili na kukaidi amri ya Wizara ya Madini.

Kesi hiyo inamkabili mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite Arusha, Joel Mollel “Saitoti” na wafanyakazi wake sita kuhusu tukio la Machi 13 mwaka huu katika mgodi uliopo kitalu B unaomilikiwa na kampuni ya Gem & Rock Venture.

Mwendesha Mashitaka wa serikali, Mosses Hamilton,mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Charles Uiso alidai kuwa katika kesi hiyo serikali itawasilisha vielelezo 11 na mashahidi 24 katika kesi mbili.

Hamilton alidai shitaka la shambulizi inayowahusu washitakiwa sita akiwemo Petro Exsaud (48) mkazi wa Moshono Arusha, Mosses Kelerwa (45) mkazi wa Mirerani, Daniel Siyaya (44) mkazi wa Ilboru Arusha, Mosses Sirikwa (46) mkazi wa Ilboru, Dausen Mollel (58) mkazi wa Ilboru na Enock Nanyaro (32) mkazi wa Arusha itakuwa na mashahidi 16 na vielelezo sita.

Mwendesha mashitaka huyo alidai shitaka la kukaidi amri ya Wizara ya Madini linalomkabili Saitoti na Nanyaro litakuwa na mashahidi wanane na vielelezo vitano.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walizuiwa kufanya shughuli za uchimbaji lakini walikaidi na kuendelea na kazi.

Katika maelezo ya awali Hamilton alidai kuwa Machi 13 mwaka huu wafanyakazi sita wa Gem & Rock Venture waliwashambulia watumishi wa taasisi za serikali na wafanyakazi sita wa kampuni ya Franone inayochimba Kitalu C  wakiwemo Benson Banash ,Vedastus Swea, Alvin Msuya, Swetbert Albogast, Mussa Unambe na Bonfance Mollel na kuwajeruhi usoni.

Washitakiwa hao walikana maelezo ya awali na dhamana yao iliendelea kwa kila mshitakiwa kudhaminiwa na mdhamini na bondi ya shilingi milioni moja. Kesi ilihairishwa hadi Mei 10 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.

Habari Zifananazo

Back to top button