UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kusafirisha kilogramu 1001.17 za dawa za kulevya aina ya Heroin inayomkabili mkazi wa Mikocheni Hussein Hariri na wenzake wawili, umedai kuwa wanatarajia kuwa na vielelezo sita na mashahidi saba.
Wakili wa serikali Caroline Matemu amedai hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio.
Matemu alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, ambapo wanatarajia kuwa na mashahidi saba pamoja na vielelezo sita.
Alidai kuwa vielelezo hivyo ni hati za kusafiria, gari mbili, simu tano, dawa za kulevya aina ya Heroin, ripoti ya mkemia mkuu pamoja na ripoti ya ukamataji.
Hakimu Mrio alisema anaahirisha kesi hiyo hadi mahakama kuu itakapowaita kwa ajili ya kuanza usikilizwaji na washitakiwa watendelea kubaki rumande.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Benson Muro (32) mkazi wa Mbezi na Ramadhani Almas (46) mkazi wa Magomeni Mapipa.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 17 mwaka 2022, eneo la Mbezi Chini.
Inadaiwa kuwa bila halali washitakiwa hao walikutwa wakisafirisha kiasi hicho cha dawa za kulevya aina ya heroin kinyume cha sheria.