Mashindano ya Qur’an kutamatika Aprili 5

DAR ES SALAAM: Mashindano ya Tuzo za Kimataifa za Qur’an Tukufu yanatarajiwa kufikia kilele chake Jumapili, Aprili 5, huku washiriki kutoka mataifa 25 wakianza kuwasili nchini kushiriki tukio hilo kubwa la kidini linaloendelea kupata umaarufu kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Othman Kaporo, amesema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika, na zoezi la mapokezi ya washiriki limeanza rasmi tangu alfajiri ya leo.

Kaporo ameeleza kuwa ujio wa washiriki utaendelea hadi Ijumaa, huku wakitarajia kupokea washiriki wote kutoka mataifa mbalimbali. Amesema mwaka huu mashindano hayo yanashirikisha nchi 25 kutoka nje ya Tanzania, na kufanya jumla ya nchi 26 kushiriki tukio hilo.
Amefafanua kuwa hatua ya nusu fainali itafanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, uliopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kuanzia saa mbili asubuhi hadi jioni, ambapo washiriki bora watachujwa kuingia hatua ya fainali.
Ameongeza kuwa mgeni rasmi katika hatua hiyo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kuhusu fainali, Kaporo amesema zitafanyika katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa, jijini Dar es Salaam, na kutoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuenzi tukio hilo muhimu la kidini.

Aidha, amebainisha kuwa mashindano hayo yatapambwa na uwepo wa wageni mashuhuri wa kidini kutoka nje ya nchi, wakiwemo Maimamu kutoka Makkah na Madina watakaoongoza dua maalum kwa ajili ya kuiombea nchi, viongozi wake na wananchi.
Kaporo pia amesema mashindano hayo yatasimamiwa na jopo la majaji wa kimataifa, likiongozwa na Sheikh kutoka Saudi Arabia atakayekuwa Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, Sheikh Hassan Chizenga, akizungumza kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Bin Zubeir, amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo, akisisitiza umuhimu wake katika kuimarisha mshikamano na maadili ya kiimani.
Ameeleza kuwa sehemu ya nusu fainali itakayofanyika Zanzibar itarushwa mubashara kupitia kituo cha televisheni cha ZBC ili kuwapa fursa Watanzania wengi zaidi kufuatilia mashindano hayo.
Sheikh Chizenga amesisitiza kuwa mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia Qur’an Tukufu, na kuifanya nchi kuwa kitovu cha matukio ya kidini yenye mvuto wa kimataifa.
Ameongeza kuwa tukio hilo linaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee duniani kwa kukusanya maelfu ya watu wanaokusanyika kusoma, kusikiliza na kuenzi Qur’an Tukufu, jambo linaloleta fahari kwa taifa.
Akihitimisha, ametoa wito kwa Watanzania wote, bila kujali dini zao, kushiriki katika tukio hilo ili kupata baraka na kuendelea kuimarisha amani, akieleza imani kuwa Mungu ataibariki Tanzania na kuizidishia mafanikio.



