Mashindano ya uchoraji yaibua vipaji shuleni

DAR ES SALAAM: WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema mashindano ya kazi za sanaa ya uchoraji yaliyoandaliwa kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam yamekuwa chachu ya kukuza vipaji vya vijana na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa maonyesho hayo yaliyofahamika kama ‘Tanzania On Canvas, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Profesa Daniel Mushi, amesema mashindano hayo ni matokeo ya juhudi za Ubalozi wa India katika kuunga mkono maendeleo ya vijana kupitia sanaa.

Amesema jumla ya shule 30 ziliingia kwenye mashindano hayo ambapo shule 10 zilipata washindi wa kuendelea katika michuano inayofuatia jambo ambalo linaonyesha mshikamano na utayari wa walimu kushika mkono wanafunzi wao.

Michoro iliyowasilishwa imeonyesha historia ya Tanzania, maliasili ikiwemo mbuga za wanyama, utamaduni pamoja na mawazo ya vijana juu ya namna wanavyoiona nchi yetu kupitia macho ya sanaa kilele cha mashindano hayo kitafanyika Oktoba 4, mwaka huu.

Profesa Mushi amesema lengo la mashindano siyo ushindani pekee bali ni jukwaa la kuwafanya wanafunzi waonyeshe vipaji vyao na kutumia ujuzi huo kama fursa ya kujikwamua kiuchumi.

Rais Samia Suluhu Hassan mwaka huu alizindua sera mpya ya elimu na mafunzo yenye mambo makuu matatu; kuongeza elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi kumi, kuwepo kwa michepuo miwili mikuu ikiwemo wa amali unaowawezesha wanafunzi kupata ujuzi, na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kujifunzia.

Alisisitiza kuwa uchoraji uko chini ya mchepuo wa amali, hivyo wizara itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha vijana wanapata ujuzi utakaowaondoa kwenye utegemezi na hatimaye kuchangia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Aidha, aliishukuru Ubalozi wa India kwa mchango wake katika kuendeleza vipaji vya sanaa na utunzaji wa utamaduni wa kitanzania kupitia michoro ya vijana.
Kwa upande wa balozi wa India nchini, Bishwadip Dey amesema mshindi wa kwanza atapata Sh milioni 2.5, wa pili milioni 2,wa tatu milioni 1.5,washindi wa tuzo za faraja watapata milioni 1 kila mmoja na washiriki wengine watapata Sh 100,000 kama zawadi na kutambua juhudi zao.

Dey amewahimiza wanafunzi kuendelea kukuza vipaji vyao vya ubunifu sambamba na masomo yao, na kushiriki kwenye shindano kwa furaha bila hofu ya kushindwa, kwani ni fursa bora kwa maendeleo yao binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button