Mashine za ushirika Chato zauzwa chuma chakavu

WANACHAMA wa Chama Cha Ushirika Chato (CCU) wameazimia kuivunja bodi ya chama kufuatia tuhuma za kuuza bila ruhusa vyuma chakavu kutoka baadhi ya mashine ya viwanda vimavyomilikiwa na chama.

Azimio hilo limefikiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa saba wa CCU uliofanyika wilayani Chato Mkoa wa Geita baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa awali kutoka ofisi ya Mrajis mkuu wa vyama.

Akisoma taarifa ya uchunguzi wa sakata la uuzaji wa mali za chama, Ofisa Mrajis Msaidizi Mkoa wa Geita, Menace Chandika amesema uchunguzi ulifanyika kuanzia Desemba 30, 2024 hadi Januari 3, 2025.

Amesema uchunguzi umejiridhisha kuwa uuzaji wa vyuma, haukupata ridhaa ya ofisa Mrajis wa vyama vya ushirika na mkutano mkuu wa wanachama badala yake ilijadiliwa na bodi ya wanachama pekee.

Chandika amesema vyuma hivo vilikuwa na uzito wa Kg 14,680 na viliuzwa kwa thamani ya sh milioni 11 badala ya thamani halisi ya sh milioni 11.27 katika biashara ambayo haikuhusisha ofisi ya utathimini ya serikali.

“Mali ziliuzwa bila kufuata utaratibu kinyume cha kifungu namba 60 (2) cha jedwali la tatu, kifungu kidogo cha 1a cha sheria ya vyama vya ushirika namba 6 ya mwaka 2013.

“Pia imebainika mkataba unaonyesha vyuma vimenunuliwa na Sayona Company Limited, lakini mnunuzi wa mwisho anatoka Nyakato Mwanza ambaye anamiliki yadi ya kuhifadhia na kuuza vyuma chakavu”, amesema Chandika.

Ameongeza kuwa, kutofanyika kwa tathimini kunafanya mali hizo kutoakisi thamani halisi ya vyuma hivyo huku malipo yakipokelewa kama fedha taslimu kinyume cha taratibu za kihasibu.

Chandika amesema pia uchunguzi umebaini mkataba wa mauziano ni wa kugushi (feki) kwani vyuma havikuuzwa kwa kampuni ya Sayona Company Limited kama inavyoonekana kwenye mkataba huo.

Ameongeza pia mkataba haukushuhudiwa na mwanasheria yeyote, mkataba hauna mhuri wa chama na wanunuzi, na biashara ilifanyika kwa matakwa binafsi yasiyozingatia maslahi mapana ya chama.

Awali Mweyekiti wa CCU, Johnson Kilimokwanza aliyesimamishwa Februari 28, 2025 amesema vyuma viliuzwa kwa Baraka zote za bodi ili pesa itakayopatikana itumike kulipia eneo la kiwanda cha ushirika.

Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kuwajibika kwa kuzingatia maslahi ya chama ili kuepuka mgawanyiko, kudhoofisha umoja na kuathiri ufanisi wa ushirika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button