Mastaa, mikopo mitandaoni vinara malalamiko taarifa binafsi

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC) imesema imesajili taasisi 1,850 zinazokusanya na kuchakata taarifa na nyingine 300 zipo katika hatua za kujisajili.

Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Stephen Wangwe alisema hayo mjini Morogoro juzi wakati wa kujibu maswali ya wahariri kwenye warsha ya wahariri kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Alisema usajili huo utakoma Aprili 30, mwaka huu.

“Kuanzia mwezi Mei mwaka huu, tume itaanza kusimamia sheria ili kuhakikisha taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa zinajisajili na kusimamia ulinzi wa taarifa binafsi,” alisema Wangwe.

Alisema pia PDPC imepokea na kushughulikia malalamiko yasiyopungua 60 yakiwemo ya utoaji taarifa za watu waliohusika kwenye mikopo ya mitandaoni na watu maarufu kulalamikia taarifa na picha zao kuhusika kwenye matangazo bila idhini zao.

Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dk Emmanuel Mkilia alisema PDPC inaendelea na mikakati ya kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha sheria zinasomana ili kuondoa ukinzani wa kisheria kati ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na sheria nyingine.

Alisema kutokana na mijadala iliyojitokeza katika warsha hiyo na mafunzo, zinahitajika hatua za pamoja kati ya PDPC na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ili kuimarisha faragha na ulinzi wa taarifa binafsi kwa manufaa ya jamii ya Watanzania.

Dk Mkilia alisema tume hiyo inapendekeza kuwe na ushirikiano wa karibu kati ya tume na TEF ili kuhakikisha kuwa elimu kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi inafika kwa wanahabari wote na inajumuishwa katika sera na maadili ya vyombo vya habari.

“Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinajisajili tume na kuwa na maafisa wa ulinzi wa taarifa binafsi na kuonesha kwa jamii ya kimataifa, kikanda na hapa nchini kuwa vyombo vya habari vya Tanzania vinazingatia faragha na ulinzi wa taarifa binafsi,” alisema.

Dk Mkilia alisema ni muhimu PDPC na TEF waandae Mwongozo wa Vyombo vya Habari kuhusu Ulinzi wa Faragha na Taarifa Binafsi.

Alisema mwongozo huo utasaidia kutoa mwangaza wa kimaadili na kisheria katika uandishi wa habari ili kuzuia uvunjaji wa haki za faragha za watu na hivyo kulinda faragha hizo na taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria bila kuingilia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata habari.

Dk Mkilia alisema pia ni muhimu kuwe na mafunzo ya mara kwa mara kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na kanuni zake.

“Hili ni jambo muhimu na tukishirikiana elimu hii itawafikia waandishi wote wa habari nchini na kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya kuiga katika kulinda faragha na ulinzi wa taarifa binafsi,” alisema.

Dk Mkilia alisema pia ni muhimu kuanzisha dawati la kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa faragha ndani ya vyombo vya habari.

“Hili litasaidia kuhakikisha kuwa malalamiko yanayohusiana na uvunjifu wa faragha yanashughulikiwa kwa haraka na kwa haki ndani ya vyombo vya habari, vyama vya wanahabari na taasisi zote zinazofanya kazi kuhakikisha sekta ya habari na mawasiliano kwa umma inakuwa kinara wa kusimamia haki za faragha na ulinzi wa taarifa binafsi,” alisema.

Dk Mkilia alitaja jambo lingine ni kufanya tafiti za pamoja kati ya PDPC, TEF na taasisi za kihabari nchini na vyombo vya habari ili kuelewa changamoto zinazoikumba sekta ya habari katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda faragha za watu na taarifa binafsi, kupendekeza suluhisho sahihi kwa sekta ya habari bila kuathiri majukumu na matakwa ya sheria na kanuni za sekta ya habari nchini.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile aliishukuru PDPC kwa kundaa mafunzo kwa wahariri na akaahidi kuwa jukwaa hilo lipo tayari kushirikiana na tume hiyo kufanya tafiti, kuandaa mwongozo wa vyombo vya habari na uanzishwaji wa madawati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button