MGANGA Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Dk Hussein Yahya amesema wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na matatizo ya ngozi, sababu kubwa ni matumizi ya vipodozi visivyofaa kiafya.
Aidha, amesema changamoto ya kutokuwa na wataalamu wa ngozi wa kutosha inasababisha watu wengi kushindwa kupata huduma sahihi ya matibabu hayo.
Katika mahojiano na HabariLEO, Dk Yahya ambaye ni mtaalamu wa tiba ya ngozi alisema utumiaji wa vipodozi vyenye viambata vya sumu kwa asilimia kubwa umeathiri ngozi za watu wengi hasa akina dada.
Alisema tatizo la vipodozi linatibika na njia mojawapo ni kuacha vipodozi vyenye athari.
Alifafanua kwamba anapokutana na mgonjwa ambaye tatizo lake la ngozi limetokana na vipodozi, kwanza anachofanya ni kujua kipodozi alichotumia na kitu kilichosababisha tatizo lake.
Alisema baada ya kujua hutoa elimu kwa mgonjwa na kumshauri kuacha kukitumia na kisha humpatia tiba sahihi.
Alisema katika Hospitali Kuu ya Polisi ya Rufaa Kilwa Road mkoani Dar es Salaam, wamekuwa wakikutana na akina dada walioathirika na vipodozi kwa wingi katika kliniki zao na vingi ni vile vilivyopigwa marufuku na serikali.
“Kwa mahudhurio ya kliniki moja kwa sababu tuna kliniki mbili kwa wiki. Tuna takribani wagonjwa wasiopungua 30 mpaka 40 wenye shida ya ngozi na katika hao utagundua kuwa karibuni robo au zaidi ya robo ni madhara yatokanayo na matumizi ya vipodozi,” alisema.
Mtaalamu huyo alishauri katika kipindi hiki cha likizo na sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ambapo watoto wako nyumbani, wazazi wasiwahusishe watoto wao na matumizi ya vipodozi wanavyovitumia.
Kuhusu upungufu wa madaktari wa magonjwa ya ngozi, alisema imesababisha watu wengi kwenda kwenye duka la dawa na kununua na kutumia pasipo ushauri wa daktari.
Hali hiyo amesema imesababisha wengi kutumia dawa ambazo si sahihi kulingana na matatizo yao.
Comments are closed.