DAR ES SALAAM: MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango anatarajiwa kuongoza matembezi ya hisani Julai 20 yenye lengo la kuchangia kampeni ya Okoa Mlima Kilimanjaro ya upandaji wa miti ya kutosha kuhifadhi mlima huo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Nessa iliyoandaa matembezi hayo Deborah Nyakisinda amesema katika mkutano na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo kwamba miti miti bilioni 1 inahitajika kwa ajili ya kurejesha uhalisia wa mlima huo na kuwahimiza wadau kujitokeza kwa wingi kuunga mkono kampeni hiyo.
“Ni wajibu wa kila mmoja kuulinda mlima huu sio kwa watu wa Kilimanjaro pekee yake bali Watanzania wote kwa kuwa ni mlima wetu sote,” amesema.
Isome pia:https:https://habarileo.co.tz/ummy-kufanya-mazoezi-na-mimi-ruksa/
Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema uhalisia wa Mlima huo ndio unaofanya kuvutia wengi kwenda kutembelea na kuongeza fedha za kigeni hivyo, Watanzania hawana budi kuungana kuokoa.
Amesema Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam itachangia sh milioni moja kwa ajili ya kununua miti na kuhimiza wadau wengine kujitokeza kusaidia kampeni hiyo ya Okoa Mlima Kilimanjaro kuchangia upatikanaji wa miti ya kutosha.
“Ukipanda Mlima wa Kilimanjaro utaona athari iliyotokana na moto, pia theluji imepungua tunatakiwa kuurudisha ule uhalisia wake, tunachofanya ni kushirikiana na Nessa Foundation na Tanapa katika kampeni hii ili kuuokoa,”amesema.
Naye Mhifadhi Mkuu Mfawidhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Hassan Nguluma amehimiza jamii inayozunguka Mlima Kilimanjaro kuona umuhimu wa kulinda mazingira ya mlima huo.
Wengine walioahidi kuchangia kampeni hiyo ni Mfuko wa UTT sh milioni tatu huku benki ya Maendeleo ikiahidi kuchangia miti 50.
Awali, Mkurgenzi wa NESSA, Nyakisinda alisema matembezi yatakuwa ya km 5, 10 na 16 kuanzia geti la Marangu na kuishia Mandara.