Matukio makubwa mwaka 2024: Rais Samia aweka historia G20

MWAKA 2024 Tanzania iliandika historia nyingine baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupata mwaliko wa kushiriki mkutano mkubwa wa nchi tajiri duniani maarufu kama G20 kutoka kwa Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva.

Hii ni mara ya kwanza kwa mkuu wa nchi kutoka Tanzania kushiriki katika mkutano huo. Awali Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na yule wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete walishiriki mkutano kama huo, wakati huo ukifahamika kama G8 kabla haujafanyiwa mabadiliko yaliyotokea mwaka 2008.

Hivyo basi, Rais Samia anakuwa mkuu wa nchi wa kwanza na mwanamke wa kwanza Afrika kushiriki katika mkutano wa G20 uliofanyika kwa siku mbili katika Jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil.

Advertisement

Mkutano wa G20 huzikutanisha nchi tajiri duniani ambazo zinachangia asilimia 85 ya pato la dunia pamoja na asilimia 75 ya biashara za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Novemba 15, mwaka huu ilisema kuwa Rais Samia amealikwa katika mkutano huo kushiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa ya na umasikini, kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.

Shauku ya wengi katika huo mkutano ni kusikia ni nini Afrika ama rais huyu mwanamke atakisema katika mkutano huo, macho na masikio yakaelekezwa kwake.

Rais Samia katika mkutano huo alikwenda na kupigilia msumari ajenda yake ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Alizitaka nchi tajiri kuunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ili kuokoa mazingira.

Akizungumza na wahariri, Rais Samia alisema kupata nafasi ya kutambulika na kuitwa ni mafanikio makubwa.

“Sisi si wanachama wa G20, lakini wameona haja ya kutualika kama Tanzania kushiriki kwenye mkutano huu. Ushiriki wetu una manufaa makubwa kama Tanzania, lakini kama Afrika,” alisema. 

Mafanikio ya mkutano huo

Kilimo: Baada ya mkutano huo, Rais Samia alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini ambapo kampuni kutoka Brazil zimeonesha nia ya kuwekeza nchini katika sekta ya kilimo.

“Kwa muda mrefu Tanzania tunanunua mbolea kutoka nje. Ndani pale tuna viwanda viwili, kile cha Intracom na kile cha Minjingu lakini bado tunaagiza mbolea kutoka nje, kwa hiyo sasa kazi yetu ni kuvutia wawekezaji wa mbolea kuja kuweka viwanda ndani halafu tuweze kuzalisha na tusambaze kwa wakulima wetu,” alisema.  

Nishati jadidifu: Katika masuala ya nishati jadidifu kumeonekana mwelekeo baada ya Rais Samia kufanya mazungumzo na Rais wa Misri ambaye naye alizungumzia masuala ya Bwawa la Julius Nyerere lakini kama kawaida, akikutana na Misri kubwa wanalozungumza ni matumizi mazuri ya Mto Nile.

Rais Samia pia, alisema katika hili aliipa nafasi ajenda ya nishati safi ya kupikia.

“Nilikutana na Waziri Mkuu wa Norway, tunashirikiana katika masuala ya nishati safi, tulikubaliana tuendelee na mikakati yetu kuhakikisha Afrika kunapatikana umeme wa kutosha,” alisema.

Pia alisisitiza, “Lengo letu ni kwamba ikifika mwaka 2030 karibu watu milioni 300 kati ya milioni 700 Afrika wawe wamepata umeme, hilo ndio lengo”. 

Biashara: Mafanikio katika masuala ya biashara ni pamoja na kuzungumza na Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto ambapo alisema, “Indonesia tulisaini nao mkataba mambo ya biashara, kwa hiyo tukawa tunazungumza jinsi ya kutekeleza huo mkataba, kubadilishana ziara za wafanyabiashara kwenda Indonesia na kuja Tanzania.”

 Miundombinu: Mkutano huo umeleta neema katika maendeleo ya miundombinu hapa nchi baada ya Rais Samia kukutana na Taasisi ya Kibenki ya Maendeleo ya Miundombinu kutoka Asia (AIIB) inayolenga kutoa mikopo ya kuboresha miundombinu.

“Tanzania tumeona haja ya kuingia kwa sababu ile benki inasaidia fedha za ujenzi wa miundombinu kwa hiyo Tanzania tumeingia uanachama,” alisema.

Katika mkutano huu, Rais Samia pia alikuwa mmoja wa waliopitisha azimio la muungano wa kimataifa la kupinga umasikini na njaa pamoja na azimio la matumizi ya nishati safi.

Mkutano wa G20 ulijadili ajenda kuu tatu ambazo ni utawala bora, maendeleo endelevu na matumizi ya nishati safi pamoja na kuondoa njaa na umasikini duniani.