MATUKIO MAKUBWA MWAKA 2024: Ujasiri wa Dk Tulia waonekana IPU
DAR ES SALAAM; 2024 ni mwaka ulioambatana na matukio makubwa yaliyoweka historia katika nyanja za siasa, ikiwa ni pamoja na ushindi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson kushika nafasi ya urais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Dk Tulia anakuwa rais wa 31 wa umoja huo akiwa ni mwanamke wa tatu kushika nafasi hiyo ambaye alipatikana kwa kura ya siri iliyopigwa na wabunge wapatao 700 kutoka mataifa 130 duniani.
Aliwashinda wagombea wengine watatu kwa kupata asilimia 57 ya kura katika awamu ya kwanza ya upigaji kura.
Katika kinyang’anyiro hicho kwa mara ya kwanza Afrika ilipeleka wagombea wanne wanawake kushiriki na Dk Tulia akaibuka mshindi dhidi yao akiwa ni mwanamke wa tatu kushika wadhifa huo akitanguliwa na Najma Heptulla wa India na Gabriela Cuevas wa Mexico lakini wa kwanza kwa Afrika.
“Naikubali nafasi hii kwa unyenyekevu wote, huku nikitambua majukumu yanayoambatana nayo,” alisema Dk Tulia baada ya kutangazwa mshindi.
“Ninathibitisha tena dhamira yangu ya kufanya kazi pamoja nanyi nyote ili kuifanya IPU kuwa shirika lenye ufanisi zaidi, linalowajibika na lililo wazi,” aliongeza akionesha ushupavu na hali ya kuaminika katika kuitumikia nafasi hiyo.
Ushindi huo pia ulimgusa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X alimpongeza, Dk Tulia na kusema kuwa ushindi wake ni ushuhuda wa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, na imani walionayo wajumbe juu yake na nchi ya Tanzania.
Yapo baadhi ya makundi ya wakosoaji duniani waliotoa maoni ya kuonesha, Dk tulia hakustahili kuishika nafasi hiyo lakini yeye hakutetereka.
Nguvu yake katika IPU iliendelea kuonekana ya kawaida sana mpaka Oktoba 14, mwaka huu alipofungua mkutano wa 149 wa umoja huo na kukutana na maswali yaliyoonekana kutaka kumdhoofisha kwenye nafasi yake, lakini Dk Tulia alibaki imara.
Sakata hilo lilianza kwa Mwakilishi kutoka Lithuania kuuliza ni nani aliyempa (Dk Tulia) mamlaka ya kuiwakilisha IPU nchini Urusi na ziara hiyo ilikuwa na faida gani ya kidemokrasi kwa IPU kinyume na kutumiwa kama propaganda ya Urusi?
Kwa hali ya kuonesha kukerwa na kwa ushupavu mkubwa, Dk Tulia alilipangua swali hilo kwa kueleza namna alivyotuma barua kwa mataifa hayo mawili kutoa taarifa ya nia yake ya kutaka kufanya ziara na kueleza sababu za kwenda Urusi kabla ya Ukraine.
“Barua zilitumwa kwa pande zote mbili Ukrane na Urusi lakini nilipanga kuanza ziara yangu nchini Ukraine hata hivyo Serikali ya Ukraine ilijibu kuwa Rais na Spika wa bunge katika tarehe hizo wangehudhuria mkutano wa Nato, New York, hivyo haikuwezekana kunikaribisha kwa wakati huo,” alisema.
Alisema hakuwa na uwezo wa kuzuia mpango huo na alilazimika kufanya ziara yake Urusi huku akihoji kuwa kama ni suala la mamlaka, ni nani alimpa rais aliyepita wa umoja huo, Duarte Pacheco mamlaka ya kwenda Ukraine.
“Rais aliyepita alitembelea Kieve, nani alimpa mamlaka hayo, tafadhali nadhani tufike mahali ambapo nimejieleza vya kutosha mara nyingi kwenu na kwa kila mmoja ambaye anataka kuelewa,” alisema.
Aliwataka wabunge hao wamuamini kama ambavyo waliona inafaa yeye kuwaongoza na aliendelea kuwa imara kwa kipindi chote cha mkutano mpaka alipoufunga Oktoba 17 mwaka huu, kwa hotuba iliyosisitiza umoja kwa mabunge ya dunia.



