Matukio mwaka 2024; Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi yazinduliwa

 DAR ES SALAAM; APRILI 3, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Tume hiyo ilianzishwa Mei Mosi, mwaka jana baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11, 2022.

Wakati anaizindua katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam Rais Samia alisema itavutia mitaji nchini na kukuza uchumi shirikishi wa kidijitali.

Advertisement

Alisema Tanzania ina kila sababu ya kutunga sheria na kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kutunza haki ya faragha kwa kila mmoja hasa katika kipindi hiki cha kukua kwa teknolojia.

“Kwa kuzingatia maendeleo ya kiteknolojia taarifa binafsi za watu zinaweza kukusanywa, kuchakatwa na kutumika bila hata wahusika kufahamu hiyo haikuwa sawa,” alisema Rais Samia.

Alisema licha ya taarifa binafsi kutumika kwa hujuma pia ni biashara kwenye kampuni za kimtandao hivyo ni muhimu kulindana kupitia sheria ili zisitumike vibaya.

Rais Samia alisema serikali imeamua kuweka utaratibu wa kisera na kisheria ili kulinda taarifa binafsi zinazochakatwa, kuhifadhiwa na kusambazwa ili kulinda haki ya faragha, jambo ambalo pia ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Tanzania imekamilisha uandaaji wa Sheria tatu za msingi ambazo ni Sheria za Makosa ya Mtandao 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa ya mwaka 2022.

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na.11 ya mwaka 2022 inaweka utaratibu wa kulinda haki ya faragha ya mtu kama ambavyo imebainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 16 (1) (2) na Ibara ya 15 ya Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo katiba zote mbili zinazungumzia haki ya faragha na usalama wa mtu.

Pia, kuwepo kwa Sheria hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ibara ya 61 (b) ambayo imeelekeza kuongeza ufanisi na usiri wa Taarifa za wananchi katika mawasiliano kwa kutunga Sheria ya kuimarisha ulinzi wa taarifa na takwimu. 

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa binafsi ni mahususi kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa lengo la kuweka kiwango cha chini cha matakwa ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi, kuanzisha Tume ya ulinzi wa Taarifa Binafsi, kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ina majukumu likiwemo la kusimamia utekelezaji wa sheria, kusajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi na kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko kuhusu madai ya ukiukwaji wa ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu.

Pia, tume hiyo ina jukumu la kufanya tafiti na kufuatilia maendeleo ya Teknolojia kuhusiana na uchakataji wa taarifa na kuimarisha ushirikiano na nchi zingine.