Matumizi maarifa ya asili yakimbiza mabadiliko ya tabianchi

MATUMIZI ya maarifa ya asili katika uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji na mazingira umesaidia jamii ya wafugaji Kata ya Enguserosambu wilayani Ngorongoro kutoathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakizungumza na waandishi wa habari  waliofika katika kata hiyo kupitia mradi wa uhifadhi mazingira kwa maarifa asilia ambao unatekelezwa na taasisi ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) kwa kishirikiana na taasisi ya CILAO katika mradi unaodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) kupitia programu ya miradi midogo na kuratibiwa na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) baadhi ya viongozi wa mila na serikali wameeleza matumizi ya maarifa ya asili yameleta ufanisi mkubwa.

Viongozi hao wa mila na serikali katika Kata ya  Enguserosambu, walieleza kuwa sheria kali imesababisha kata hiyo kuwa na msitu mkubwa wa asili  wenye hekta 14,700.

Kiongozi wa mila, Parmitoro Pumbani alisema wamekuwa na sheria ya mila kutoza faini ya ndama jike, kulaaniwa  ama kunyang’anywa mke kwa ambao watabainika kukata miti ama kuharibu mazingira.

Pumbani alisema faini hizo zimesababisha kata yao kuwa ya mfano katika utunzwaji wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili.

Naye Katibu wa Bodi ya Msitu wa Enguserosambu, Marko Tarash alisema msitu wao umekuwa na faida kubwa kwa jamii kwani wana uhakika kupata malisho ya mifugo mwaka mzima,kupata dawa za asili,matunda, maji na kuni za kupikia.

Tarash alisema msitu huo unaundwa na vijiji vinne ambavyo ni Enguserosambu,Ng’arwa, Orkiu na Naan.

Awali Ofisa Mtendaji Kijiji cha Enguserosambu, Duni Mollel alisema uwepo sheria za mila umesaidia uhifadhi kwani Wananchi wanaziheshimu zaidi.

Mwalimu, Edward Sasi wa Shule ya Msingi Enguserosambu alisema licha ya kuwepo elimu ya kisayansi lakini nao wao katika shule wamekuwa wakisisitiza wanafunzi kuzingatia elimu ya asili katika uhifadhi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button