Matunda miaka 60 ya Muungano

DAR ES SALAAM; Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 2024.

“TUNAPOFIKIA Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania tunaongozwa na Rais mwanamke mbobezi Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan na nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika pande zote mbili za Muungano.” Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama anatoa kauli hiyo Aprili 8, mwaka huu mjini Dodoma katika uzinduzi wa Nembo na Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isemayo: Miaka 60 ya Muungano Tumeshikamana, Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”.

Anasema: “Kwa mara ya kwanza Tanzania inajivunia kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Dk Samia Suluhu Hassan… Hili ni jambo la kujivunia maana ni Rais mbunifu, mwenye uwezo wa hali ya juu na aliyethibitisha ndani na nje ya nchi kwa utendaji kazi wake uliotukuka”.

Kwa mujibu wa Jenista, Watanzania wanajivuna kutimiza miaka 60 ya Muungano ukiwa na ‘matunda’ mengi ya kihistoria, kijiografia, kitamaduni, kibiashara, kisiasa na kiusalama ambayo yameendelea kuwaunganisha watu wa Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika) kama taifa moja la Tanzania.

Advertisement

“…Hii ni Jubilei ya almasi, hatuna budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha kwa furaha kubwa,” anasema. Licha ya mafanikio lukuki, zipo pia changa moto ndogondogo zinazotokana na uelewa wa mambo kwa baadhi ya watu wakiwamo hasa baadhi ya wanasiasa.

Katika Kongamano la Tathmini ya Miaka 60 ya Muungano lililoandaliwa na Mchambuzi Media na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) na kufanyika Unguja, Zanzibar, baadhi ya wanasiasa, wanazuoni na wachambuzi wa mambo ya kihistoria na kisiasa wanataja faida za Muungano.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Wanasema ni pamoja na kupanuka kwa maeneo na fursa za kibiashara, kiuwekezaji na kiuchumi, kudumisha udugu na umoja wa kitaifa, kuendeleza Kiswahili, Tanzania kupata heshima kubwa kimataifa pamoja na kuimarika kwa amani, umoja, ulinzi na usalama Bara na Visiwani.

Balozi Amina Said anasema yapo matunda mengi ya Muungano japo mengine hayaonekani kwa macho. Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Idd Mandi anasema Muungano umeleta amani na kupanua wigo wa kibiashara.

Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda wa UDSM anasema adui mkubwa wa Muungano ni umaskini ambao baadhi ya watu wanauhusisha na Muungano jambo ambalo si sahihi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyeongoza uzinduzi wa nembo na kaulimbiu ya maadhimisho anasema, Watanzania hawana budi kuwashukuru viongozi wao kwa kuwezesha Muungano kufikia miaka 60 wakiwa na umoja na mshikamano wa kitaifa.

“…Hakuna mwananchi ambaye hajafikiwa na faida za Muungano… Muungano wetu ni wa udugu, wananchi wengi wameunganisha udugu, urafiki na wengine wameoleana…”

“Pamoja na misingi ya kisiasa, hakuna anayeweza kuvunja udugu wa damu uliopo. Tulianza kuchanganya udongo sasa tuna mchanganyiko mkubwa wa damu,” anasema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo anasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) katika Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Urais wa Dk Hussein Mwinyi zimetatua hoja 15 za Muungano kati ya 18 kwa miaka mitatu.

Machi 5, mwaka huu, Jafo alinukuliwa katika Kikao cha Mawaziri wa SJMT na SMZ kujadili masuala ya Muungano kilichofanyika Nyamanzi, Zanzibar akisema serikali hizo zimefanikiwa kutatua hoja 22 za Muungano kati ya 25 zilizokuwepo awali.

Akataja hoja zilizobaki kuwa ni suala la sukari, usajili wa vyombo vya moto, bodi ya pamoja na mgawanyo wa mapato ya iliyokuwa sarafu ya pamoja ya Afrika Mashariki.

Anaungana na Watanzania wengine kuwapongeza Rais Samia na Dk Mwinyi kwa kazi kubwa wanayofanya kulinda Muungano.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Nyamanzi, Zanzibar hivi karibuni, Dk Mwinyi anasema SJMT na SMZ zinachukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.

Kwa nyakati tofauti anasema juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali zikiwamo za kuunda tume na kamati kushughulikia hoja za Muungano ikiwamo Kamati ya Serikali ya SJMT na SMZ kushughulikia masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006, zinadhihirisha serikali hizo zinavyojitahidi kushughulikia na hatimaye kumaliza hoja hizo.

Imebainika kuwa, tangu mwaka 2006 hadi 2024, hoja 22 kati ya 25 zilizopokewa na kujadiliwa, zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Mwinyi anasema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024, hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya 18 zilizokuwapo na kwamba, utatuzi wa changamoto za Muungano umeongeza imani ya Watanzania kwa serikali zao, hivyo kuuimarisha na kudumisha amani na utulivu wa Tanzania ambao ni tunu na fahari muhimu ya nchi. Hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.

Kupitia vyanzo mbalimbali, imebainika kuwa, Watanzania wana imani kubwa kuendelea kupata matunda zaidi ya Muungano kutokana na utashi uliopo na dhamira ya dhati ya serikali zote katika Muungano kwani zinafanya jitihada kubwa kuzipatia ufumbuzi hoja zilizobaki.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/hoja-22-muungano-zapatiwa-ufumbuzi/

“Nawahakikishia wananchi wote wa Tanzania, kwamba serikali zote mbili zitaendelea kuchukua hatua ili nchi yetu iendelee kupiga hatua za maendeleo na ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu,” anasema Dk Mwinyi.

Anaongeza: “Katika kipindi cha miaka 60, Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote. Muungano wetu umeipa heshima kubwa nchi yetu katika Jumuiya ya Kimataifa”. “…Umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu katika shughuli mbalimbali unaongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu”.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Hamza Hassan Juma anasema Watanzania waendelee kudumisha Muungano ambao ni tunu iliyowekwa na waasisi wa Muungano Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume.

“Miaka 60 ya kuungana kwetu ni jambo la kujivunia. Hadi sasa Watanzania chini ya uongozi wa Rais Samia na Dk Mwinyi wanaendelea kuimarisha Muungano wetu,” anasema.

Kwa mujibu wa Hamza, ni wajibu wa kila Mtanzania kuulinda, kuutunza na kuutetea ili Muungano uendelee kudumu na kuwafanya Watanzania waishi kwa amani na usalama zaidi.

Anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania Aprili 26, 1964, umedumu na kuendelea kuimarika kutokana na viongozi wa pande zote kujadili kwa uwazi changamoto zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja.

Anatoa mfano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoundwa na nchi nane inayoendelea kudumu kutokana na kutumia uzoefu wa Tanzania kama moja ya mafanikio lukuki ya Muungano wa Tanzania. Vyanzo mbalimbali vinasema historia ya Tanzania imeundwa na sababu nyingi hadi kufikia kusainiwa kwa hati ya Muungano mwaka 1964 chini ya waasisi wa taifa, Nyerere na Karume.

Baadhi ya sababu hizo vyanzo vinasema ni urafiki na udugu wa damu wa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar, lugha ya Kiswahili iliyowaunganisha watu wa pande hizo na vyama vya ukombozi vya TANU (Tanganyika African National Union) na ASP (Afro Shiraz Party) vilivyotoa mchango mkubwa katika Muungano.

Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela anakanusha madai ya wachache waliohofu kwamba Zanzibar ‘itamezwa’ kama kutakuwa na mfumo wa serikali moja akisema hofu yao haikuwa ya msingi. “Hili ni suala la wakati tu. Kwa wakati huo, ni kweli ingeweza kuonekana kwamba, labda Tanganyika itaimeza Zanzibar, lakini wakati ule si sawa na wakati wa hiki kizazi kipya.

Sioni vipi Mzanzibari wa sasa ataona anamezwa na Tanzania; anamezwaje?” Anahoji. Anaongeza: “Naamini suala la kumezwa lilikuwa wakati ule tunaanza, lakini tumeufikisha Muungano mahali ambapo Mtanzania wa Bara na Mzanzibari wote tunajiona kitu kimoja, kwa hiyo unapojiona ni kitu kimoja suala la kusema fulani anammeza fulani halipo.”

Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Zanzibar, Nadra Mohamed anasema ili kuendelea kuimarisha Muungano, serikali ijitahidi kuondoa kero chache za muungano zilizobaki.

“Changamoto ni kawaida hata nyumbani zipo na kimsingi, Muungano kama muungano Watanzania tumeshauweza, haturudi nyuma tena waliosema hatuuwezi, tayari tumeshauweza tuna wajukuu na vitukuu sasa,” anasema Nadra.

Anasema kutokana na busara za Rais Samia na Dk Mwinyi, hoja za muungano sasa zimebaki tatu. Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib anasema, kadiri kero za Muungano zinavyomalizika, ndivyo Muungano unavyozidi kuimarika na kufanya iwe vigumu kuvunjika.

/* */